Wakati baadhi ya watu wakificha makabila yao kwa kuhofia aibu zinazotokana na utani wa makabila. Ndugu wawili Leah Ndahani na Pendo Hukwe wao wameamua kutumia lugha ya kabila lao la Wagogo kujiingizia kipato kwa njia ya muziki.
Ndugu hao ambao ni mtu na shangazi yake waliounda kundi lao la The Zawose Queens, wamejikuta wakinufaika na lugha ya kigogo huku wakiiambia Mwananchi ni vyema kwa wazazi kurithisha tamaduni kwa watoto wao.
"Zawose ni jina la familia maana yake ni 'wa wote' ipo kwenye lugha yetu ya kigogo. Mimi nilianza kuimba tangu nikiwa na miaka 14. Nilivyokuwa mdogo sana nilianza huu muziki familia yetu sisi ni wanamuziki nilikuta babu na baba wakifanya hivyo na mimi nikaingia kwenye.
"Huyu pembeni yangu ananiita shangazi. Kwenye kundi kwa sasa tupo wawili tu lakini tulianza kwenye kundi la nyumbani, la familia lililokuwa linaitwa Chibite kwa hiyo sisi tumeanzia kwenye mzizi wa Chibite,"amesema Pendo Hukwe.
Hata hivyo, wamesema mapokezi ya watu kuhusiana na muziki wao ni mazuri kwani wanavyoimba wapo ambao hawaelewi kigogo lakini wanawapa ushirikiano.
"Kupitia muziki huu tumepata mafanikio mengi ikiwemo, tunashiriki matamasha mengi kama vile ya huko UK na tumepanda majukwaa mengi kama Echolot Festival, Explore The North Festival na mengine. Muziki wetu tunachanganya tunaimba Kigogo lakini kuna vyombo vingine vinachanganya kama gitaa hiyo yote ni kuweka ladha pamoja.
"Wanawake wengi tumekuwa waoga kufanya kitu, mimi nawaambia wanawake wenzangu ni vyema kukitoa kipaji kionekane maana anaweza kupata msaada wa kusaidiwa.
"Sisi tumejipanga tunamuomba Mungu tusishindwane, maana makundi mengi yanaenda kisha yanabomoka,"wamesema.
Wamesema changamoto wanayokutana nayo ni watu wengi kupenda zaidi miziki ya nje kuliko ya asili zao.
"Bongo Fleva ipo juu zaidi kuliko sisi tunaofanya muziki asili. Kwa sababu hata jamii, tumejikuta sanaa yetu ya asili tumeiweka nyuma.
"Nafikiri watu wengi waache ushamba. Wakubali vya kwao kwa sababu nyumbani ni nyumbani. Hiyo inakuwa ni ushamba na haujikubali. Watu wajikubali wakubaliane na hali zao,"wamesema.

Leave a Reply