Msanii wa Hip Hop Marekani, Megan Thee Stallion (30) na mpenzi wake mpya, Klay Thompson (35) ambaye ni mchezaji wa kikapu katika timu ya Dallas Mavericks, wameonekana kwa mara ya kwanza hadharani tangu kuthibitisha uhusiano wao.
Wawili hao waliambatana pamoja Jumatano hii, Julai 16, wakipita katika zulia jekundu la hafla ya hisani ya Pete & Thomas Foundation Gala iliyoandaliwa na Megan jijini New York.
Akiwa amevalia gauni jeusi lenye shingo ya halter na mkanda wa fedha, Megan alifanya mahojiano ya kipekee na mtandao wa People na kueleza jinsi walivyokutana na Klay pamoja na lengo la kuandaa hafla hiyo ya kurudisha katika jamii.
"Tulikutana kwa namna ya kipekee sana, kama kwenye filamu vile. Sitakuambia ilikuwaje wala lini, lakini ilikuwa kama sinema, na yeye naweza kusema kuwa ni mtu mzuri zaidi niliyekutana naye maishani mwangu." alisema Megan.
Kauli ya Megan inakuja wiki moja tu baada ya kumtambulisha Klay kwenye ukurasa wake wa Instagram hapo Julai 9 ambapo aliposti mfululizo wa picha kadhaa ikiwepo yake na Klay.
Katika picha hiyo, rapa huyo kibao, Body (2020), anaonekana ameketi kwenye jakuzi, huku upande wa kushoto Klay akiwa amelala kwenye kiti akiota jua. Megan aliambatanisha picha hiyo na emoji ya mti wa mnazi na emoji ya ndege.
Kuhusu tukio hilo la hisani, kwa mujibu wa tovuti ya taasisi hiyo, wanalenga kukusanya rasilimali fedha ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wanawake, watoto, wazee na jamii zisizopata huduma stahiki huko Houston na duniani kote.
Taasisi hiyo ambayo imepewa jina la wazazi wa Megan ambao ni marehemu kwa sasa, Joseph Pete III na Holly Thomas, programu zake zinalenga maeneo ya elimu, makazi, afya na ustawi wa jamii.
"Nahisi kama wanaona ninachokifanya sasa hivi. Nahisi kama wananitazama kutoka mbinguni na kusema, ‘Ndiyo binti yetu!’ Nahisi kama mama yangu anafurahia sana." alisema Megan na kuongeza.
"Naona kama anapiga makofi. Nahisi kama bibi yangu pia anafurahia. Baba yangu nahisi anasema, ‘Hivi ndivyo nilivyotarajia mtoto wangu afanye.' Nahisi wanajivunia sana mimi." alisema Megan.
Mwaka 2020, Jarida la Time kwenye orodha yao ya kila mwaka, lilimtaja Megan kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi dunini.
Ikumbukwe Megan Thee Stallion jina lake lilianza kuwa kubwa kimuziki baada ya kutoa wimbo wake, Hot Girl Summer (2019) akiwa na Ty Dolla Sign na Nicki Minaj, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kusainiwa na lebo ya 1501 Certified Entertainment.
Megan aliandika rekodi katika tuzo za 63 za Grammy kama rapa wa pili wa kike kushinda kipengele cha Msanii Bora baada ya Lauryn Hill kufanya hivyo mwaka 1999.
Hata hivyo, wakati huo Lauryn Hill kupitia albamu yake, The Miseducation Of Lauryn Hill (1998) alishinda Grammy tano, kikiwemo kipengele cha Albamu Bora ya Hip Hop akiwa ni mwanamke wa kwanza katika historia kufanya hivyo.
Na pia albamu hiyo ilishika namba moja chati ya Billboard 200 na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa Hip Hop duniani kufanya hivyo, kisha akafuata Foxy Brown, Chyna Doll (1999) na Eve, Let There Be Eve... Ruff Ryders' First Lady (1999).

Leave a Reply