Peter Akaro
Jumatano hii mastaa wa Bongo Fleva, Billnass (32) na Nandy (33), waliadhimisha miaka mitatu tangu wamefunga ndoa na kufanya harusi ya aina yake ambayo iliteka mazungumzo mjini na mitandaoni kwa sana.
Miaka mitatu ndani ya ndoa yamejaliwa kupata mtoto mmoja, Naya (2022) ambaye ni maarufu katika mitandao ya kijamii akiwa na wafuasi zaidi ya 746,000 katika ukurasa wake Instagram unaosimamiwa na wazazi wake.
Ikumbukwe Billnass na Nandy waliofunga ndoa Julai 16, 2022 katika kanisa la KKKT Mbezi Beach, Dar es Salaam, ikiwa ni takribani miaka saba tangu kuanza kwa uhusiano wao kwa mara ya kwanza.
Walisoma pamoja CBE ila hawakuwa na ukaribu, sasa wote walipokuja kufanya vizuri kimuziki, wakaitwa katika tamasha la Fiesta 2016, wakaenda kutumbuiza Sumbawaga ila wakaenda kulala Mbeya na huko ndipo historia ikaanza kuandikwa.
Uhusiano wao waliendelea kuufanya siri mbele ya mitandao na vyombo vya habari hadi mwaka 2020 walipochumbiana na kuja kufunga ndoa Julai 2022, ikiwa ni miezi michache kabla ya Nandy kujifungua.
Hadi sasa wamefanikiwa kupingana na hata kuishinda ile dhana kuwa wanamuziki wanapooa au kuolewa ushawishi wa sanaa yao hushuka kutokana na kupoteza mvuto kwa mashabiki wengi lakini kwao nyimbo kubwa zaidi zimetoka baada ya ndoa.
Mathalani, Billnass ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) kwa mara ya kwanza na kutoa nyimbo zilizopata namba kubwa katika majukwaa ya kidijitali kuliko zote za mwanzo akiwa bachela.
Ikiwa ni takribani miaka tisa tangu alipotoka na wimbo wake, Raha (2014), Billnass alishinda tuzo ya TMA kwa mara ya kwanza katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022.
Katika TMA 2015 na 2021, hakushinda ila baada ya kuingia tu katika ndoa, basi ikawa baraka kwa kushinda mbele ya wakali wa Hip Hop kama Fid Q, Joh Makini, Country Wizzy na Kala Jeremiah.
Utakumbuka ushindi huo ulikuja baada ya Billnass kufanya vizuri na wimbo wake, Puuh (2022) ulioweka rekodi kama wimbo wa Bongo Fleva uliosikilizwa zaidi Boomplay Music 2023 ukiongoza chati kwa wiki sita.
Hadi sasa wimbo huo aliomshirikisha Jay Melody, ndiyo wimbo pekee wa Billnass aliosikilizwa zaidi Boomplay, pia ndiyo wimbo wake ambao video yake imefanya vizuri zaidi YouTube ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 16.
Na mwaka huo wa ndoa, Billnass alikuwa msanii wa pili wa Hip Hop Bongo aliyetazamwa zaidi YouTube, video zake zilitazamwa zaidi ya mara 25.9, huku akiwa ametanguliwa na Darassa aliyetazamwa mara milioni 28.6.
Mwaka 2021, alifungua lebo yake, Mafioso Inc ambayo imekuwa ikisimamia kazi zake, hatua hiyo ni baada ya kufanya kazi na Rada Entertainment, L.F.L.G (Live First Live Good) na Rooftop Entertainment.
Naye mkewe Nandy, licha ya kuanzisha lebo yake, The African Princess miaka mingi nyuma, hakuweza kumsaini msanii yeyote ni hadi pale alipoingia kwenye ndoa ndipo akamsaini Yammi, 23, hapo Januari 2023.
Wazo la kufungua lebo lilianza tangu Nandy alipoachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) chini ya Epic Records inayomilikiwa na Sony Music Entertainment, kampuni tanzu ya Sony Corporation of America.
Yammi ambaye ameachana na lebo hiyo miezi mitatu iliyopita, chini ya usimamizi wa Nandy alijiunga na kampuni kubwa ya usambazaji muziki Afrika na India, Ziiki Media yenye ushirikiano na Warner Music Group.
Baba Levo aliwahı kumkosoa Nandy akıdaı baada ya kufunga ndoa ameshindwa kutoa wimbo uliofunika zaidi, ila Nandy hakujali, bali alitulia na kuja na wimbo wake, Dah! (2024) akimshirikisha Alikiba kutokea Kings Music.
Ndani ya mwaka mmoja tu, video ya wimbo huo imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 24 ikiwa ni video pekee ya Nandy iliyofanya vizuri zaidi katika jukwaa hilo kwa muda wote.
Kabla hajaolewa hakuna wimbo wake uliyoweka rekodi hiyo, hata ule wa kwanza kumshirikisha Alikiba, Nibakishie (2020) uliotoka miaka minne iliyopita hadi leo haujafikia hata nusu ya namba hizo.
Ikumbukwe Billnass ameshiriki kuandika wimbo huo wa Nandy, Dah! (2024), na kwa ujumla wawili hao wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024).
Hii ni couple nyingine ya mastaa Bongo ambayo imefanya kolabo nyingi zaidi baada ya Navy Kenzo (Nahreel na Aika) ambao wametoa albamu tatu, AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023).
Kundi la Navy Kenzo lilianzishwa Aprili 2013 ingawa walikuwa pamoja kimuziki tangu mwaka 2008 walipokuwa wanasoma India, walianza kufanya vizuri katika kundi la Pah One na baadaye kuondoka na kuanzisha Navy Kenzo, couple yenye watoto wawili.
Leave a Reply