Akili bandia kuanza kufundisha wanafunzi masomo ya maabara

Akili bandia kuanza kufundisha wanafunzi masomo ya maabara

Ukweli ni kwamba sayansi na teknolojia imekuza sekta nyingi kama vile biashara , elimu na nyingineze.

Kwenye ulimwengu wa sasa wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijifunza vitu mbalimbali kupitia mitandao.

Katika kuendeleza jitihada za kuboresha na kukuza elimu nchini, kampuni ya SmartDarasa imekuja na maboresho mapya katika mfumo wake.

Maboresho hayo ni pamoja na kupata material ya darasani kwa njia ya matumizi ya akili bandia na kusoma notes za darasani hata kama hakuna huduma ya mtandao wa intaneti.

Mfumo ambao unafahamika kama SmartDarasa 2.0 ambao umepangwa kuanza kazi Julai 1, 2024, utawawezesha wanafunzi kujifunza kwa urahisi masomo ya STEM kupitia komputa na simu janja.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika ofisi za Smartlab, Juni 7, Afisa Mkuu wa Operesheni kutoka SmartDarasa, Faith Silaa, alisema ya kwamba mfumo huu mpya utawawezesha wanafunzi kuelewa zaidi.

"Kwa kutumia nguvu ya akili bandia, SmartDarasa 2.0 inalenga kubadilisha umakini wa wanafunzi kutoka kwenye kujifunza kwa kukariri hadi kuelewa kwa kina, hivyo kuchochea uzoefu zaidi wa kujifunza," alisema Faith.

Hata hivyo, Faith alitilia mkazo juhudi za muda mrefu za SmartDarasa katika kurahisisha elimu, akieleza mikakati iliyotekelezwa kwa kuongeza uelewa na kuwafunza wanafunzi kutumia mfumo mpya kwa ufanisi.

"Kupitia ziara za shuleni na miradi ya majaribio, SmartDarasa itahakikisha wanafunzi wanapata rasilimali bora zilizopo, ikithibitisha uaminifu wake kwa ubora wa elimu," alieleza Faith.

Mkurugenzi wa Utafiti, Habari, na Machapisho katika Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Kwangu Zabron, alisifu jitihada za SmartDarasa kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha elimu nchini.

"Katika elimu ya msingi hadi sekondari, matumizi ya ICT yamezingatiwa sana kwa sababu mfumo unajukumu kubwa katika kuboresha elimu katika sekta zote. Hivyo, uwepo wa wadau kama SmartDarasa ni wazi kuwa ni maono ya Rais Samia na Wizara ya Elimu katika kuwaleta pamoja wadau wa teknolojia ya habari na mawasiliano," alisema Masalu.

Hata hivyo, Zabron aliendelea kusema kuwa ni wakati sasa kwa wadau wa ICT kufanya kazi na serikali.

"Sasa ni wakati sahihi kwa wadau wa teknolojia ya habari na mawasiliano kufanya kazi pamoja na serikali katika kusaidia elimu nchini, kusaidia watoto wa Kitanzania ili wakimaliza viwango vyao husika vya elimu, wawe na uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi," alieleza.

Afisa Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, David William, alisisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja kati ya wizara kuboresha mfumo wa elimu kupitia ICT.

"Kulikuwa na wakati ambapo kila mtu alikuwa akifuata njia yake—Wizara ya Elimu, TAMISEMI, na Wizara yetu ya ICT. Hivyo, tukaamua kufanya mkutano wa pamoja ili wadau wote waweze kuungana. Tunakuja na kitu kinachoitwa Edunet. Katika hii, wadau wote wataweza kushirikiana kufikia hadhira kubwa kwa kasi moja," alisema.

Toka kuanzishwa kwake mwaka 2019, SmartDarasa imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa shule ambazo zinachangamoto ya maabara kupata nafasi ya kujifunza maabara kupitia mfumo wa Augmented Reality (AR).

Hii ikiwa na maana ya kwamba inaonyesha teknolojia inayochanganya vitu vya kweli na vya kidijitali katika mazingira ya mtumiaji ili kuboresha uelewa na uzoefu wa mazingira hayo.

Takribani watu elfu ishirini kutoka nchini, Kenya, Nigeria, India na Marekani wamepata nafasi ya kujifunza kupitia mfumo huu.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post