Albamu Mpya Ya Nandy 2025 Ina Maana Gani

Albamu Mpya Ya Nandy 2025 Ina Maana Gani

Na Peter Akaro

Staa wa Bongofleva, Nandy tayari ametangaza ujio wa albamu yake ya pili ambayo inatarajiwa kutoka mwaka huu ikiwa ni miaka tisa tangu alipotoka kimuziki na kibao chake, Nagusagusa (2016) chini ya Tanzania House Talent (THT).

Nandy anayefanya vizuri na wimbo wake mpya, Mlete (2024), unakuja na albamu hiyo baada ya kutoa EP tatu, Taste (2021), Maturity (2022) na Wanibariki (2021) yenye muziki wa Injili pekee.

Utakumbuka albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) chini ya Epic Records ilitoa nyimbo maarufu kama Aibu, Hazipo n.k, huku ukijumuisha ambazo tayari zilikuwa zimetoka kama One Day, Wasikudanganye, Kivuruge na Ninogeshe.

Je, albamu hii mpya ya Nandy ina maana gani kutoka mwaka huu wa 2025 na kipi hasa tutarajie?, kuna mengi ya kuzungumza katika eneo hilo ila kwa sasa tutagusi haya matano yafuatayo.

Mosi; Nandy amefanya hivyo ili kuepuka kutoa albamu ndani ya mwaka mmoja na mshindani wake wa karibu, Zuchu ambaye kwa sasa anafanya vizuri na albamu yake mpya na ya kwanza, Peace and Money (2024) yenye nyimbo 13.

Nandy anajua kivyovyote vile Zuchu hawezi kutoa tena albamu 2025, hivyo uwanja wa kujidai utakuwa wake peke yake, hiyo ni sawa na Diamond Platnumz aliyetoa EP, First of All (2022) baada ya hasimu wake kimuziki, Alikiba kutoa albamu, Only One King (2021).

Ikumbukwe ukiachana na Zuchu, wasanii wengine wa Bongofleva waliotoa albamu 2024, ni Roma (Nipeni Maua Yangu), Jay Melody (Therapy), Young Lunya (Mbuzi), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop), Marioo (The Godson), Rayvanny (The Big One) n.k.

Pili; Hii ni albamu ya kwanza kwa Nandy tangu kushinda tuzo nne za Muziki Tanzania (TMA) 2021 & 2023 akiwa ni msanii wa pili wa kike aliyeshinda mara nyingi zaidi tangu msimu wa 2021 nyuma ya Zuchu alishinda tuzo saba hadi sasa.

Nandy ameshishinda vipengele vingi vikubwa katika TMA kama Msanii Bora wa Kike ila cha Albamu Bora ya Mwaka ndio bado na hajawahi kuwania, hivyo huwenda mradi huo mpya ukampa nafasi hiyo hapo mwakani kama kweli utatoka kama alivyotangaza.

Ukiachana na TMA, Nandy ameshishinda tuzo nyingine kama Maranath Awards 2018, AFRIMA 2017 & 2020, AMI Awards Africa 2018, AEAUSA 2021, AFRIMMA 2021 na The Orange Awards 2023 ambazo ni maalumu kwa wasanii wa kike.

Tatu; Pia itakuwa ni albamu ya kwanza tangu ameanza kusaini wasanii katika rekodi lebo yake, The African Princess akianza na Yammi aliyetambulishwa kupitia EP yake, Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu na bila kolabo yoyote.

Yammi aliyewania TMA 2023 kama Msanii Bora Chipukizi, tangu ametambulishwa amefanya vizuri, mathalani wimbo wake, Tiririka (2023) video yake imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 10 YouTube, rekodi ambayo wasanii wengi wakubwa hawana.

Hivyo ni wazi Nandy ameona mwaka mmoja baada ya kusimamia mradi wa Yammi na kuwa na matokeo mazuri, ni wakati sahihi kuja na wake, pia tuturajie kuwa Yammi atakuwepo katika albamu hiyo baada ya kushirikiana katika wimbo, Lonely (2024).

Nne; Nandy mwenye EP tatu, anakuja na albamu ya pili wakati mume wake Billnass ambaye alitanguliwa kutoka kimuziki kabla yake kupitia wimbo wake, Raha (2014) chini ya Rada Entertainment, akiwa hajawahi kutoa EP wala albamu!.

Pengine albamu hii mpya ya Nandy itaweza kumuamsha Billnass na kumkumbusha kuhusu hilo, ni mara chache sana msanii kuwepo katika muziki kwa miaka zaidi ya 10 akifanya vizuri lakini hatoi EP au albamu kwa mashabiki wake.

Hata hivyo, Bilnass, mmiliki wa lebo ya Mafioso Inc, naye anatarajiwa kuwepo katika albamu hiyo ya Nandy, huo utakuwa ni wimbo wa sita kushirikiana baada ya Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024).

Tano; Jay Melody ni msanii mwingine Bongo anayetarajiwa kusikika katika albamu hiyo baada ya kumaliza tofauti zao za muda mrefu na Nandy alishathibitisha kuwa kuna kazi yao inakuja mwaka huu.

Na hiyo ni baada ya Jay Melody kumwandikia Nandy nyimbo nyingi na zote zikafanya vizuri, Jay kamwandikia nyimbo nne ambazo ni Kivuruge (2017), Njiwa (2018) ft. Willy Paul, Hallelujah (2019) ft. Willy Paul na Do Me (2020) ft. Billnass.

Ikumbukwe mume wa Nandy, Billnass alishinda tuzo yake ya kwanza ya TMA kufuatia kumshirikisha Jay Melody katika wimbo, Puuh (2022) na kushinda kama Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022 akiwabwaga Kala Jeremiah, Country Wizzy, Fid Q na Joh Makini.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags