Mwigizaji kutoka nchini Afrika Kusini ambaye alipata umaarufu kupitia tamthilia ya Isidingo, Don Nawa amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66.
Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na familia yake mapema jana Jumatano Aprili 16,2025 huku sababu ya kifo chake haikuwekwa wazi.
“Ni kwa uchungu mkubwa tunaposhiriki habari za kifo cha baba yetu mpendwa, Don Mlangeni-Nawa, [aliyefariki dunia] tarehe 16 Aprili 2025.
“Alikuwa moyo wa familia yetu, baba mwenye upendo, kaka, na rafiki. Kwa dunia, alikuwa mwigizaji mwenye kipaji na anayeheshimika ambaye uwepo wake uliangaza kila jukwaa na skrini aliyokuwa juu yake,” inasomeka taarifa hiyo.
Kwenye tamthilia ya Isidingo, Don Nawa alikuwa akifahamika kwa jina la Zebedee Matabane (maarufu kama Zeb Matabane). Alikuwa mmoja wa wahusika wakuu na waliopendwa sana katika mfululizo huo wa televisheni.
Aliacha kuoneka katika Tamthilia hiyo Aprili 29, 2014, baada ya kutumika kwa zaidi ya miaka 15 kama Zebedee "Zeb" Matabane huku kukiwa na tetesi kuwa kuondoka kwake kukiwa ni kutokana na mzozo wa nidhamu na kampuni ya Endemol South Africa pamoja na mtayarishaji wa tamthilia hiyo.
Mbali na Isidingo Nawa amewahi kuonekana kwenye filamu nyingine mbalimbali ikiwemo The Throne, Hlala Kwabafileyo, Isidingo – The Need, na Sgudi Snaysi.

Leave a Reply