Kesi inayomkabili Rapa A$AP Rocky imeendelea kupamba moto mahakamani huku ikidaiwa kuwa mwanamuziki huyo huwenda kuna siri anaificha ambayo hataki ifichuke.
Kwa mujibu wa tovuti ya TMZ wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo ya shambulio mapema jana Ijumaa Februari 7, 2025 Rocky alimzuia rafiki yake A$AP Twelvyy, asijibu swali aliloulizwa na mahakama.
Waendesha mashtaka walimhoji Twelvyy kwa kumuonesha picha ya kitanda cha Rocky kilichoandikwa "AWGE" na kumuuliza maana yake ni nini lakini kabla Twelvyy hajajibu, Rocky alipaza sauti, "Usiseme!"
Kitendo hicho kilisababisha hali ya mtafaruku, Twelvyy alijibu tu, "Inamaanisha AWGE," jambo lililomkasirisha mwendesha mashtaka, ambaye alimwomba jaji amlazimishe shahidi huyo kuwa mkweli zaidi. Twelvyy aliendelea kukaidi, na ndipo wakili wa Rocky, Joe Tacopina, akaomba mazungumzo ya faragha na jaji.
Hatimaye, Rocky alipata alichotaka kwani Twelvyy hakufichua maana ya zile herufi nne, inadaiwa kuwa AWGE ni shirika la ubunifu lililoanzishwa na Rocky mwaka 2014, huku kanuni yake namba moja ikiwa ni ‘Kamwe usifichue maana ya AWGE’.
ASAP Rocky, anakabiliwa na mashtaka mawili ya uhalifu, akidaiwa kumpiga risasi rafiki yake wa zamani na mshirika wa kundi la muziki la ASAP Mob.

Leave a Reply