Fahamu Tatizo La  Umeme Wa Moyo Uliokuwa Ukimtesa Mbosso

Fahamu Tatizo La Umeme Wa Moyo Uliokuwa Ukimtesa Mbosso


Baada ya video za mwanamuziki Mbosso kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwa hospitali amelazwa. Msanii huyo ameweka wazi kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la Umeme wa Moyo kwa muda mrefu lakini kwa sasa amepona kabisa.

"Kwa sasa kijana wenu nimepona kabisa ugonjwa wa moyo uliokuwa unanisumbua kwa kipindi cha miaka yote na jana jioni nimeruhusiwa kuendelea na mapumziko nyumbani na baada ya wiki 1 niweze kuendelea na majukumu yangu ya kila siku,” ameeleza Mbosso kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Ameeleza kuwa juzi Februari 11, 2025 ilikuwa siku ya hofu kwake, mashabiki na kwa familia yake. Lakini alifanikiwa kupatiwa matibabu ndani ya saa moja na sasa amepona kabisa.

Hata hivyo, ikumbukwe mwanzoni mwa 2024 katika moja ya mahojiano yake, Mbosso aliweka wazi kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa miaka mingi. Na kuongezea kuwa jambo hilo lilikuwa likiathiri baadhi ya mambo katika maisha yake kama vile ratiba ya kazi, mazoezi na vyakula.

Aidha wakati akizungumza na Mwananchi, Prof Harun Nyagori ambaye ni daktari Bingwa Mshauri Mwandamizi wa magonjwa ya ndani na moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. Alipoulizwa kuhusu mtu kupona umeme wa moyo, alisema inategemeana chanzo na sababu na aina ya ugonjwa wa moyo unaogundulika kwa huyo muathirika.

"Kuna matatizo ambayo mtu anayozaliwa nayo yanaweza yakatibika kwa haraka mara tu anapowahi kabla hajawa mtu mzima. Ila kuna mengine huwa yanasubiri mtu awe mtu nzima baadaye anapandikizwa umeme wa bandia ili kuwa wa kudumu au kupewa kifaa maalumu kuthibiti umeme kuongezeka au kupungua. Na huduma zote hizi zinapatikana hapa kwenye taasisi yetu ya moyo Jakaya Kikwete,"amesema.

Amesisitiza jambo muhimu ni mtu yeyote mwenye dalili ya kuona giza ghafla na kudondoka, kizunguzungu cha ghafla, moyo kwenda mbio au kupoteza fahamu ni vyema akawahishwa kwenye taasisi kwa uchunguzi zaidi na wa haraka.

"Ni vyema watu kufanya vipimo vya mara kwa mara, kwani ugonjwa huo ni mbaya kwani muda mwingine wagonjwa wanaweza kupoteza maisha ghafla bila hata dalili, watu wasikariri kuwa tatizo linaweza likasubiri muda,"amesema.

Fahamu kuwa umeme huo husaidia kusukuma damu na kupeleka kwenye viungo mbalimbali. Hivyo basi tatizo la umeme wa moyo ni pale mapigo ya moyo yanapokuwa chini sana au juu sana hali ambayo si ya kawaida.

"Mapigo ya moyo yanakuwa chini ya 40 kwa dakika. Mgonjwa anapata shida anapokuwa anafanya shughuli zake anachoka au wakati mwingine anaanguka na anapata shida sana," aliwahi kunukuliwa Dk Kisenge wakati akizungumza na Mwananchi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags