James Cameron ni mmoja wa waandishi, waongozaji, na watayarishaji wa filamu maarufu duniani. Huku akijulikana zaidi katika kutengeneza filamu kubwa zilizopata mafanikio na mauzo kama Titanic, Avatar, na Terminator.
James alizaliwa 16 Agosti 1954, Canada. Alisomea Fizikia na baadaye Fasihi ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha California, Fullerton lakini hakuweza kumaliza masomo yake.
Historia yake katika kupenda filamu
Cameron alianza kupenda filamu akiwa mtoto, hasa baada ya kutazama filamu ya kisayansi iitwayo '2001: A Space Odyssey' (1968) iliyoongozwa na Stanley Kubrick. Filamu hii ilimvutia na kumfanya avutiwe na teknolojia ya filamu na hadithi za kisayansi.
Wakati akiwa kijana, umri ambao alihitaji kupata kazi kwa ajili ya kumuendeshea maisha yake ndipo akaanza kujifunza kutengeneza filamu kwa kutumia kamera ya Super 8 na mara baada ya kujifunza hilo, ndipo akaamua kuandika filamu yake ya kwanza fupi yenye dakika 12 iitwayo 'Xenogenesis' (1978).
Filamu hiyo aliitengeneza akiwa na rafiki yake Randall Frakes, wakitumia bajeti ndogo ikiwa ni filamu ya kuonesha uwezo wake katika kutengeneza athari za picha (visual effects) na ilimsaidia kupata kazi Hollywood.
Baada ya Xenogenesis, alianza kufanya kazi kwenye tasnia ya filamu kama mchoraji wa modeli na athari za picha, hadi alipopata nafasi ya kuongoza filamu yake ya kwanza iitwayo ‘Piranha II: The Spawning (1982)’, ingawa filamu iliyomletea umaarufu ikiwa The Terminator (1984) ambayo pia aliandika mwenyewe.
Utajiri wake
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘Celebrity Net Worth’ Cameroon anatajwa kumiliki utajiri wa dola 800 milioni huku utajiri huo akiupata kwenye filamu zake mbalimbali akiwa mtayarishaji wa kwanza duniani filamu zake kuingiza zaidi ya dola 8 bilioni.
Filamu zake tatu ikiwemo Avatar (2009), Titanic (1997), na Avatar: The Way of Water (2022) zimeingiza zaidi ya dola bilioni 2 kila moja. Na kumfanya kuwa miongoni mwa wakurugenzi wenye mapato makubwa zaidi katika historia ya filamu.
Mbali na kazi yake ya filamu, Cameron pia anajihusisha na biashara nyingine. Yeye ni mpelelezi wa bahari na ameshiriki katika utengenezaji wa filamu za uhalisia za kina kirefu cha bahari. Pia, amechangia katika maendeleo ya teknolojia ya upigaji picha za kina kirefu na mifumo ya kamera za kidijitali za 3D.
James Cameron ameoa mara tatu huku akijaaliwa kupata watoto wanne akiwemo Josephine Archer Cameron, Claire Cameron, Quinn Cameron na Quinn Cameron, watoto watatu akiwapata kwa mke wake wa sasa Suzy Amis Cameron, aliyemuoa mwaka 2000.

Leave a Reply