Wanapotajwa mastaa wenye mchango mkubwa kwenye gemu ya Bongo Fleva, Joachim Marunda 'Master j' jina lake lazima liwepo.
Uzoefu wake kwenye gemu huku akiwa amenoa vipaji mbalimbali, umekuwa kati ya vitu vinavyompa ujasiri wa kusimama kusifia na kukosoa baadhi ya mambo kwenye kiwanda cha burudani Bongo.
Licha ya kuwa ukosowaji wake mara nyingi huzua mijadala mbalimbali mitandaoni huku baadhi ya wadau wa muziki wakidai anapenda kuingilia mambo ya watu. Mfahamu zaidi.
Master J ni mwanzilishi wa MJ Production, ambayo kwa sasa inafahamika kama MJ Records. Mkali huyo baada ya kuhitimu shahada ya uhandisi wa umeme Chuo Kikuu cha London aliamua kuweka vyeti kabatini na kugeukia sanaa kama mtayarishaji muziki na sasa amerudi kwenye taaluma yake.
Hata hivyo, baba yake ambaye alikuwa akifanya kazi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hakutaka awe mtayarishaji muziki bali afanye kazi aliyoisomea ila Master J akashikilia msimamo wake wa kuendelea na muziki hadi kuondoka nyumbani.
Kwa mujibu wa Master J, Sugu ndiye msanii wa kwanza kumlipa vizuri katika kazi hiyo, awali alikuwa anarekodi kwa Sh50,000 ila Sugu akamlipa Sh100,000 na walianza kufanya kazi kwenye albamu yake pili, Ndani ya Bongo (1996).
Mwaka 1997, akanunua gari lake la kwanza na ndipo baba yake akaanza kukubali kazi yake na sasa Master J anaheshimika na wengi kwa mchango wake mkubwa wa kuikuza Bongo Fleva huku studio yake ikirekodi albamu zaidi ya 500 kati ya mwaka 1996 hadi 2010.
Miongoni mwa nyimbo zilizorekodiwa MJ Records ni ule wa Mwana FA akimshirikisha Vanessa Mdee, Dume Suruali (2016) ambao ulitayarishwa na Daxo Chali, wasanii hao wawili nao shule ipo ila muda mwingi wameutumia katika muziki.
Hata hivyo, safari yake ya kunoa vipaji kwenye muziki wa Bongo bado unaendelea kwani ni miongoni mwa majaji katika shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search.

Leave a Reply