Waswahili wanasema bora ukosee kujenga nyumba kuliko kukosea kuoa, hilo pia aliliona mwanamitindo Jasinta Mawabe ambaye mapema mwaka huu alifanya sendoff na kuweka wazi kuwa anatarajia kuingia kwenye ndoa. Hata hivyo jambo hilo lilionekana kugonga mwamba huku akitaja sababu za kuvunja uchumba huo njiani.
Jasinta anasema wanawake wengi wanapitia unyanyasaji kwenye ndoa kwa sababu ya kupuuzia viashiria hatarishi.
“Nilikuwa naenda kuolewa nilifanya send off. Ile ndoa ya kanisani ilikuwa bado, vikatokea vitu ambavyo niliona kabisa hatuwezi kuendana nikilazimisha itakuwa mbaya zaidi. Nikaona ni bora nijiengue kabla ya ndoa kufungwa.
“Huyo mwanaume alikuwa siyo Mtanzania na maamuzi niliyochukua siyo magumu. Endapo ukijipenda na kujithamini, kuna vitu huwezi kuviruhusu kama kupigwa na kunyanyaswa. Kuna vitu utaruhusu kwenye maisha yako lakini kumbe haukustahili kuviruhusu. Wanawake wengi wanapitia magumu kwa sababu wanaogopa fulani atasema nini na jamii itasema nini,” anasema.
Anasema uamuzi huo ulikuja baada ya kugundua vitu tofauti kutoka kwa mwanaume huyo aliyekuwa mchumba wake kwa kipindi hicho.
“Unajua wanaume wapo hivi wanakuonesha kile ambacho wanataka ukione mpaka pale wakipata wanachokitaka ndiyo watakuonesha kuwa wapo hivi. Mtu anakuja anajifanya anataka kukuoa, mimi nilikuwa siishi naye kila mtu alikuwa anaishi nchini kwake.
“Nilivyoenda nikaishi kwa mwezi mmoja ndiyo nikaona kumbe alikuwa ananiigizia. Nikaona kuliko niolewe niteseka baadaye heri tuachane mapema. Mahusiano yetu yalikuwa na mwaka mmoja,” anasema.

Leave a Reply