Kademu kangu kakauchapa mtindi halafu ile fedheha ikawadia

Kademu kangu kakauchapa mtindi halafu ile fedheha ikawadia

Ilikuwa ni mwishoni mwa miaka ya 1990. Wakati huo nilikuwa nimemaliza chuo na nimeanza kuishi peke yangu baada ya kukorofishana na kaka yangu aliyenileta mjini. Nilikuwa mkorofi kiasi cha kutosha. Nilipoanza kuishi peke yangu nikawa nafanya vibarua vya hapa na pale. Lakini nilikuwa na sifa moja kubwa ambayo ni kujifanya mtu wa maana sana. Hata uvaaji wangu ulikuwa unaonesha kuwa nilikuwa kweli najimudu.

Nakumbuka vizuri kwamba, nilikuja kukumbana na msichana mmoja machachari sana ambaye baba yake alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa na maarufu hapa jijini Dar. Nasema machachari kwa sababu, alikuwa ni mtu wa matanuzi na mkwara mzito. Wiki ile nilipokutana naye, ilikuwa ni wiki ambayo, jamaa zangu fulani watoto wa kihuni walikwapua music system kadhaa, televisheni na vifaa vingine vingi tu zikiwemo kamera za video.

Kwa sababu walikuwa wanaogopa kushtukiwa kule kwao waliamua kuweka baadhi ya vitu hivyo kwenye chumba changu kwa muda huku wakitafuta wateja. Kwa hiyo chumba changu kikawa ni chumba ambacho mtu akiingia anajua kwamba, hapa kweli kuna kidume. Kulikuwa na televisheni tatu, music system nne, kamera za video mbili na vitu vingine kibao.

Wakati nakutana na msichana huyu, nilijitambulisha kama mfanyabiashara, lakini nilijiapiza kwamba nisingempeleka kwangu hata siku moja kwa sababu kachumba kangu kalikuwa kakichovu kweli. Nilitaka kutembea naye tu na kumchuna halafu basi. Lakini baada ya jamaa zangu kunijazia vitu vya wizi chumbani kwangu, niliamua kumwalika yule binti aje kwangu kwa ajili ya matanuzi na kula bata.

Yule binti alikubali mwaliko wangu na alifurahi sana, kwani nilikuwa nampiga chenga kila akizungumzia suala la kutaka kupafahamu mahali ninapoishi. Ni kweli kesho yake tuliongozana na binti huyo kwenda nyumbani kwangu. Pamoja na kwamba ilikuwa ni chumba kimoja, lakini nilijua akiona vitu vilivyomo humo ndani angezimia mwenyewe. 

Nakumbuka miaka hiyo ya mwishoni mwa 1990 ndicho kipindi ambacho vitu hivyo vilikuwa vinaonekana kuwa ujiko' mtu kuwa navyo. Yule binti alitinga kwangu na kushangaa kukuta vifaa kama vile, halafu kwenye chumba kimoja tena uswahilini! Nilimwambia, ninafanya hivi kwa usalama. Unajua vibaka wa huku Mikoroshini kwa Mpelumbe hawawezi kufikiria kwamba, chumba kimoja kama hiki kinaweza kuwa na mali. Na pia kumbuka kuwa nafanya biashara, unaweza kukuta kesho nimeshaviuza vyote.' Nilisema ili kujihami.

Tulikaa pale na yule binti kuanzia saa tano asubuhi hadi saa kumi jioni tukinywa bia na kuvunja mbavu za mbuzi. Kwenye hiyo saa kumi nilisikia hodi mlangoni. Nilienda kufungua mlango. Ile kufungua tu, nilitaka kuanguka chini kwa hofu. Hapo mlangoni kulikuwa na polisi watatu, wakiwa na wawili kati ya wale jamaa zangu walioniletea zile mali zilizokuwa mle ndani mwangu.

Hao jamaa zangu walikuwa wamechakaa, bila shaka kwa kipigo. Polisi mmoja aliuliza, ndiye huyu? Mmoja kati ya wale jamaa zangu akajibu, ndiyo'. Nilijikuta nikivamiwa na polisi wale. Nilifungwa pingu na kuongozwa ndani kwangu. Kale kademu kangu kalikuwa bado kanauchapa mtindi huku kakiwa kamejiegemeza kitandani kakiangalia tu luninga kwa raha zake. Kalipoona nimeingizwa ndani nikiwa na polisi alisimama na kusema kwa kiingereza, what is all this about, kabla hajamaliza kuongea wale polisi walikadaka.

Alitaka kufanya fujo lakini polisi walimtuliza kwa kibano. Yaani msichana mzuri kama wewe unakuwa mwizi, ajabu sana. Polisi mmoja alisema hivyo na hapo pombe zilimtoka yule binti. Mwizi! Mwizi nani? Alihoji. Wale polisi hawakumjibu. Tulipelekwa kwenye landrover  ambayo ilikuwa iko mbali kidogo na pale kwangu, na hapo ndipo majirani waliposhuhudia kidume wa mtaa nikiwa nimepigwa pingu nikiwa na kademu kangu ka kishua.

Kama mjuavyo watu wa uswahilini wasivyo na dogo, waliacha shughuli zao na kuanza kufuatilia tunakopelekwa huku kila mmoja akisema lake. Wapo waliokuwa wakinicheka kwa kejeli na kunipiga vijembe. Kusema kweli walikuwa na haki ya kunifanyia hivyo kwa sababu pale mtaani nilikuwa nasumbua sana kutokana na maringo na kujifanya matawi ya juu.

Tulifikishwa kituoni nikiwa nimeshikwa na aibu kubwa sana mbele ya kale kademu kangu. Pamoja na shughuli zangu za hapa na pale, lakini sikuwa kabisa napenda kujihusisha na wizi na nilikuwa najisikia vibaya hata ile kufikiriwa tu kwamba, ni mwizi. Sasa huyu binti ambaye aliniona mimi mtu babu kubwa, aligundua kwamba, nilikuwa mwizi. 

Yule binti alitolewa siku ile ile tuliyowekwa ndani. Si mnajua tena mzazi akiwa nazo inavyokuwa!

Hata hivyo kaka yangu na yeye alikuja kunitoa baada ya kusota Segerea kwa majuma kadhaa...






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post