Mchakato wa kurekodi ‘Hakuna Matata’ ya Marioo ulikuwa hivi....

Mchakato wa kurekodi ‘Hakuna Matata’ ya Marioo ulikuwa hivi....

Baada ya kusubiriwa kwa miezi mitatu tangu Wimbo wa ‘Hakuna Matata’ ulioimbwa na Marioo utoke, hatimaye mwanamuziki huyo ameachia video yake rasmi.

Video hiyo ambayo imefanya na waongozaji maarufu hapa nchini, Joel Malatila ‘Joma’ na Kennedy Sanga ‘Kenny’, inaonekana kutengenezwa kwa ubunifu wa hali ya juu na kubeba vivutio na utamaduni wa Kitanzania.

Akizungumza na Mwananchi, Director Joma ameeleza kuwa utengenezaji wa video hiyo umetumia siku tisa hadi kukamilika kwake huku ikiwa imerekodiwa kwenye mikoa zaidi ya minne.

"Tulitaka kuingiza uhalisia wa neno 'Hakuna Matata' ambao unamaanisha 'hakuna wasiwasi. Ili kufanikisha hilo, tulisafiri katika mikoa zaidi ya minne Tanzania, kila mkoa mmoja ulikuwa unaonesha maeneo na utamaduni wa kipekee. Ilikuwa ni changamoto lakini kitu cha tofauti," amesema.

Ameeleza kuwa video hiyo imerekodiwa maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Zanzibar na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Arusha hadi Moshi.

Aidha Joma amefichua kwamba licha ya kuwa wimbo huo unahusu mahusiano lakini video yake imebeba uhalisia wa jina Hakuna Matata.

"Wimbo ‘Hakuna Matata’ ulikuwa wa mapenzi na tulitaka kuweka mambo ya mahusiano lakini watu wanaposikia 'Hakuna Matata,' mara nyingi wanafikiria hifadhi za wanyama pori kwa hiyo tukataka kutengeneza kitu ambacho kitaendana na taswira halisi ya neno hilo,” amesema.

Muogozaji huyo amebainisha kwamba moja ya changamoto kubwa walizokutana nazo wakati wa kurekodi video ya wimbo huo ni ku-shoot video na simba kwani vifaa walivyokuwa wamebeba kwa ajili ya kurekodia, wanyama hao walikuwa wakidhania ni silaha.

Utakumbuka kabla ya kutolewa kwa video hiyo zilienea picha za Marioo akiwa na baadhi ya viongozi akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, ambapo Joma amelifafanua hilo.

"Vipande vya video ambazo Marioo alikuwa anaonesha kwa viongozi wa serikali ilikuwa ni kutoa shukrani kwa sababu kuna maeneo yalikuwa na shida tukawa tunapiga simu kwa viongozi kuomba msaada kwa hiyo ilikuwa ni kuwaonesha tumefanikiwa,” amesema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags