Msechu awanyooshea kidole wasanii wanaoimba mapenzi

Msechu awanyooshea kidole wasanii wanaoimba mapenzi

Balozi wa mazingira nchini, Peter Msechu amesema wasanii wengi wamekuwa wakitunga na kuimba nyimbo nyingi zinazohusu mapenzi badala ya kuimba mambo ya msingi yenye maslahi kwa taifa kama vile utunzaji mazingira na utalii.

Msechu ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, ameyasema hayo leo Julai 30, 2024 mjini Morogoro alipokuwa kwenye shughuli zake za muziki ambapo amesema ameamua kutumia kipaji chake katika kuisaidia serikali juu ya suala la utunzaji mazingira huku akiamini mazingira ni msingi wa maendeleo kwani bila hayo hakuna shughuli yoyote itakayofanikiwa.

"Wasanii wa sasa wengi wanaimba mapenzi, utakuta kwenye albamu nyimbo zote zinahusu mapenzi, wana kazi ya kulalamika tu kwenye nyimbo 'oooh umeniacha...oooh nakupenda' mimi siimbi nyimbo za namna hiyo," amesema Msechu.

Kuhusu mafanikio yake, Msechu amesema siri kubwa ni kwamba hana maisha ya kuigiza wakati wote amekuwa akiishi kulingana na kipato chake.

"Mimi naishi kwa kadri Mungu anavyonijalia kipato changu ndiyo kinachoamua niishi vipi na siyo mtu mwingine aniamulie niishi vile atakavyo yeye," amesema Msechu.

Amesema pamoja na kuwa balozi wa mazingira lakini amekuwa akifanya shughuli nyingine za kumpatia kipato ikiwemo bendi yake ambayo amekuwa akialikwa maeneo tofauti.

"Mimi sidharau pesa nikiitwa mahala kwenda kupiga shoo sijivungi hata kama naitwa na watu wawili mimi nakwenda ilimradi nipate pesa," amesema Msechu.

Kuhusu muonekano wake wa sasa Msechu amesema huo ndiyo anaoutaka na amekuwa akifurahia jinsi alivyo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags