Kwa niliyoyaona siku nne za tamasha la 27 la filamu za kimataifa Zanzibar 'ZIFF' nadhani yanaweza kuelezeka kwa msemo wa "ng'ombe unaweza kumpeleka mtoni lakini hauwezi kumlazimisha anywe maji".
Huo ndiyo msemo rahisi unaoweza kuelezea yaliyofanywa na baadhi ya wasanii wa Bongo Movie katika msimu huu 27 wa tuzo hizo zilizofunguliwa Agosti Mosi na kutamatika jana Agosti Tano.
Licha ya kuwa waandaaji wake walihakikisha kunakuwa na madarasa mbalimbali kwa ajili ya kunoa vipaji nchini lakini asilimia kubwa ya waliopo kwenye kiwanda cha filamu hawakuona umuhimu wake.
Zile mbwembwe za baadhi ya mastaa wa filamu kujaa kwenye kumbi mbalimbali za starehe wala hazikufanyika kwenye tamasha hilo la tuzo 2024 lililoambatana na utoaji wa mafunzo ya kukuza tasnia hiyo nchini.
Nilichokiona kwenye tamasha hilo kinasikitisha, mastaa Bongo hawakuonesha umuhimu wa kujifunza na kupata maarifa mapya kutoka kwa wataalamu na wadau mbalimbali walio katika tasnia hiyo kwani wengi wao hawakujitokeza kwenye madarasha yaliyokuwa yakitolewa na tamasha kwa ujumla.
Ni aibu kuona waigizaji, waongoza na wazalishaji wa filamu kutoka mataifa mbalimbali wakija nchini kwa ajili ya kupata mafunzo katika jukwaa hilo lakini kwa wasanii wazawa wanalipa kisogo na ndivyo ilivyokuwa.
Katika pitapita zangu nilikutana na binti kutoka Marekani ambaye alinieleza kuwa alianza kutunza pesa kwa muda mrefu ili aweze kupata nauli ya kufika kwenye tamasha hilo kwa ajili tu ya kujifunza na kukutana na watu wanaofanya kazi kama yake kwa ajili ya kupata ujuzi.
Niliyoyaona yanasikitisha, katika madarasa mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea kwa siku nne, uwepo wa hao mastaa wetu wa Kibongo ambao wangeweza kushiriki ujuzi kwa wasnii wachanga na wao kupata ujuzi mpya kutoka kwa wataalamu wa sanaa hiyo wala haukuwepo.
Wakati huo ambao madarasa yaliwahitaji sana wasanii hao kwa ajili ya kuwapa maarifa ya kukuza kiwanda cha filamu hawakuwepo badala yake, walijaa wasanii wa kigeni waliofunga safari kutoka kwenye mataifa yao tena ambayo yanamauzo makubwa ya movie kuliko kwetu.
Kwenye darasa moja jana siku ya mwisho ya tamasha ndiyo nilikutana kikundi cha baadhi ya waigizaji wa tamthilia fulani inayofanya vizuri nchini kikiwa darasani, hao ni kati ya wacheche waliofika lakini uhalisia ni kwamba waigizaji hawajajitokeza kama ilivyotakiwa.
Nadhani wakati mwingine kaburi la kufukia baadhi ya sanaa nchini linatokana na majivuno ya staa, ujuaji, kutojishusha, kutokubali kujifuza na wakati mwingine ndiyo sababu ya sanaa nchini kudumaa.
Washindi wa Tuzo za ZIFF 2024
1. UHURU WANGU (Emerson Award)
Zanzibar, imeongozwa na Mohammed Suleiman
2. OCEANMANIA/BAHARIMANIA (Best Short Film Award)
Tanzania, imeongozwa na Alphonce Haule na Gwamaka Mwabuka
3. OUR LAND, OUR FREEDOM (Best Documentary Film Award)
Kenya, imeongozwa na Zippy Kimundu na Meena Nanji.
4. GOODBYE JULIA (Best Feature Film Award)
South Sudan, imeongozwa na Mohamed Kordofani,
5. MAKULA (Best East African Film Award)
Uganda, imeongozwa na Nisha Kalema na Dan Mugisha
6. NICK KWACH (Best Actor East Africa)
Otis Janam (Kenya)
7. NISHA KALEMA (Best Actress East Africa)
Makula (Uganda)
8. JOHN ELISHA (Best Actor Tanzania)
Sozi (Tanzania)
9. JESCA MTOI (Best Actress Tanzania)
The Midnight Bride (Tanzania)
10. LIFETIME ACHIEVEMENT AWARD
Mwalimu Abdallah Mwinyi (Zanzibar)
11. ZIFF CHAIRMAN AWARDS
1. UNBANKABLE (Canada) imeongozwa na Luke William
2. MVERA (Kenya) imeongozwa na Daudi Otieno Anguka
12. SHUKRI ABDUKADIR (Best Actress Award – Tv Drama Series East Africa)
ARDAY (SOMALIA)
13. ABDALLAH MOHAMED (Best Actor Award – Tv Drama Series East Africa)
ARDAY (SOMALIA)
14. ARDAY (Best Tv Drama Series Award East Africa)
Somalia, imeongozwa na Ahmed Farah
Leave a Reply