Njia za kugundua fursa za kibiashara

Njia za kugundua fursa za kibiashara

Eenheee, niaje!! Mpambanaji na mtafutaji mwenzangu! Bila shaka huu ni wakati wakuifukuzia shilingi popote pale ilipo, usichoke endelea kupigania mkate wako wa kila siku.

Wiki hii kwenye Nipe Dili bhana nakusogezea jambo hili hapa ambalo litakusaidia zaidi katika kutambua fursa nyingi za kibiashara, fuatilia dondoo hii mwanangu mwenyewe!

Michongo yenyewe ni hii hapa kama ifuatavyo tunaanzia kwenye hili kwanza.

  • Teknolojia mpya

Yees! Hili nalo neno haswaa!! Kila kukicha kuna teknolojia mpya zinavumbuliwa ambazo kama ukiweza kuzitumia vizuri utarahisisha sana biashara uliyonayo na kuweza kuikuza zaidi.

Anza kujifunza mambo ya kibiashara na kufuatilia habari za biashara utagundua teknolojia mpya zinazoweza kuirahisha biashara yako.

Teknolojia hizi zinaweza kuwa sehemu ya kutangaza biashara, kutunza kumbukumbu na mengine mengi tu.

  • Mabadiliko yanayokuja

Angalia na hili pia suala la mabadiliko yanayotokea kila siku kwenye maisha yetu japo wengi hawapendi mabadiliko kama unataka kuziona fursa nyingi zaidi.

Anza kutegemea mabadiliko yanapotokea wewe unakuwa tayari kuweza kuwasaidia wengine kwa mabadilko hayo kupitia biashara yako. 

Epuka kuiendesha biashara yako kwa vile tu unayo biashara bali unapokuwa kwenye biashara yako fikiria ni fursa gani zipo kwenye biashara hiyo ila bado hujaziona.

Ukijiwekea tabia ya kujiuliza maswali na kujijibu mwenyewe utatambua fursa nyingi mpaka mwenyewe utakua surprised utajiuliza hivi nilikwama wapi kujua mbinu muhimu kama hizi?

  • Kitu ambacho kinafanywa ndivyo sivyo

Angalia kwenye biashara ambayo unaifanya, pia angalia wafanyabiashara wenzio wanafanya biashara zao kwa njia gani kisha utagundua kuna njia za kibiashara ambazo wengine wanafanya sivyo.

Huenda kuna huduma wanazotoa kwa hali ya chini sana, huenda wanauza bidhaa ambazo hazina viwango pia, sasa wewe unaweza kutumia nafasi hii kutoa huduma bora sana au bidhaa zenye viwango vya hali ya juu hivyo unatakiwa kuaminika ukilinganisha na wengine watapenda kufanya biashara na wewe.

  • Malalamiko ya wateja

Haya nayo ni fursa kubwa sana ukiyazingatia kwani kupitia malalamiko yao ikiwa kuna kitu ambacho hawapendezwi nacho basi una nafasi nzuri ya kukirekebisha ili wateja wakifurahie.

Kumbuka lengo lako kubwa kwenye biashara ni kutengeneza wateja wanaoiamini biashara yako shughulikia malalamiko yao kwani ni sehemu nzuri ya kukuza ulichonacho.

Safi kabisa kumbuka kuwa biashara pekee haitoshi wewe kufanikiwa, kila mtu anaweza kufungua biashara na kuiendesha lakini ni wachache wanaoweza kuona zaidi ya ile biashara waliyo nayo kuwa makini my boss.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags