Rihanna Mahakamani Kesi Ya Asap Rocky

Rihanna Mahakamani Kesi Ya Asap Rocky

Mwanamuziki maarufu wa Pop duniani, Rihanna (36) alifika mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi inayomkabili mpenzi wake na mzazi mwenzie, Asap Rocky (36) ambaye anashtakiwa kwa makosa mawili likiwemo la shambulio la bunduki.


Awali kulikuwa na taarifa kuwa Rihanna angehudhuria kesi hiyo ya jinai kwa mara ya kwanza huko Los Angeles lakini hakukua na uthibitisho wowote hadi pale ripota wa mahakama, Meghann Cuniff alipokuja kuweka wazi kuwa ni kweli alifika mahakamani.


Utakumbuka tetesi za Rihanna kuwa na uhusiano na Asap Rocky zilianza tena hapo Desemba 2019 baada ya kuonekana pamoja katika hafla ya tuzo za British Fashion na kweli ikawa hivyo na tayari wana watoto wawili wa kiume, RZA (2022) na Riot (2023).


Kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter hapo Jumatano alasiri, Cuniff alisema Rihanna alikuwa ameketi karibu na ndugu wa Asap Rocky akiwemo mama yake mzazi, Renee Black.


"Niliketi tu kwenye chumba cha mahakama kwa ajili ya kusikiliza kesi ya shambulio la bunduki, na Rihanna aliketi katika ukumbi wa mahakama karibu na mama na dada yake Asap Rocky [Erika Mayers]," alithibitisha Meghann Cuniff.


Tukio hilo linakuja katika siku ya tatu ya kusikilizwa kesi ya Asap Rocky (Rakim Mayers), mzaliwa wa New York, ambapo anashtakiwa kwa kumshambulia kwa bunduki rafiki yake wa zamani na mwanachama mwenzake wa kundi la Asap Mob, Asap Relli.


Asap Relli ambaye jina lake la kuzaliwa ni Terrell Ephron, alitoa ushahidi wake dhidi ya Asap Rocky katika siku ya pili ya kesi hiyo, akidai rapa huyo wa kibao, Fashion Killa (2013) alimtishia maisha kwa kufyatua risasi kabla ya kufika hotelini siku ya tukio.


Hata hivyo, Asap Rocky mara zote amekuwa na msimamo mkali kuhusu kesi hiyo akidai hana hatia akitaja kile kinachodhaniwa na wengi kama mkakati uliopangwa tangu awali ili kufikia lengo fulani.


"Asap Rocky ana shauku ya kutoa ushahidi wake na angependa kupata fursa ya kufanya hivyo. Yeye ni mzungumzaji sana na mwenye akili, ni binadamu mzuri na atatoka ikiwa atatoa ushahidi," alisema Wakili wake, Joe Tacopina alisema na kuongeza.


"Lakini uamuzi huo haujafanywa bado. Na inategemea jinsi kesi inavyokwenda," alisema wakili wa Asap Rocky.


Tangu mwaka 2020 Asap Rocky amekuwa akigonga vichwa vya habari hasa upande wa uhusiano wake na Rihanna, ukaribu wao ulianza kuonekana hadharani 2012 pindi walipotumbuza remix ya wimbo 'Love It' katika hafla ya utolewaji wa tuzo za MTV VMAs.


Ikumbukwe Rihanna aliyeuza rekodi zaidi ya milioni 250 duniani kote na kushinda tuzo tisa za Grammy, alipata umaarufu mkubwa baada ya kuachia albamu yake ya tatu, Good Girl Gone Bad (2007), iliyokuwa na nyimbo kali kama Rehab, Umbrella n.k.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags