Ikiwa imepita siku moja tangu mwigizaji kutoka nchini Salim Ahmedy ‘Gabo Zigamba’ kuchapisha picha kupitia ukurasa wake wa Instagram ikionesha filamu yake ya ‘Safari ya Gwalu’ ikiwa imechaguliwa na ‘Korea-Africa Foundation’ ya nchini Korea, mwigizaji huyo amefunguka sababu na vigezo vilivyotumika hadi filamu hiyo kuchaguliwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 4, 2024 kwa njia ya simu akiwa Korea, Gabo Zigamba ameweka wazi kuwa waandAaji wengi wa filamu Korea wanazingatia katika filamu za kuelimisha ndiyo maana filamu yake ya ‘Safari ya Gwalu’ imepata nafasi ya kuchaguliwa.
“Vigezo ambavyo wanachukua katika hiyo sinema ambayo umeona nimeiposti ya Safari ya Gwalu ni kwamba wanaamini sana kwenye elimu, kwa hiyo filamu yoyote ambayo ime-base kwenye elimu sana ndiyo ambazo wao wanazitazama,” amesema Gabo Zigamba.
Alichoendelea kujifunza katika ziara yake Korea
Mwigizaji huyo alifunguka zaidi kuhusiana na safari yake ya Korea ambapo ameeleza kuwa amekwenda huko kwa ajili ya kujinoa kuhusiana na masuala ya filamu huku akiweka wazi kuwa kikubwa alichojifunza ni kushikamana na wasanii wenzie.
“Mpaka leo nimejifunza mambo mengi sana, kwanza nimejifunza kujitegemea yaani kuwa na msingi wa kwamba mimi sishindwi, siwezi kushindwa na sitoshindwa, lakini kitu kingine ni kuunganisha nguvu yaani nguvu za pamoja kwa makusudi na dhamira ya kweli kwamba lazima tuungane tuweze kujenga ghorofa kwa pamoja.
"Kwa sababu ili ghorofa liweze kusimama linahitaji vitu vingi sana na hivyo vitu kila kimoja kikiwa tofauti na mwenzake basi hilo ghorofa haliwezi kujengwa kwa hiyo kwa wenzetu huku linapokuja suala la kukuza industry yao watu wanaacha kila kitu na kushirikiana, na hiki ndio kitu kikubwa ambacho nimejifunza na kinachowafanya hawa jamaa wafanikiwe kwa kiasi kikubwa katika filamu zao,” amesema Gabo Zigamba.
Aidha nyota huyo anayetamba na tamthilia ya ‘Mawio’ ametoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fursa ya kwenda Korea kwa ajili ya kuongeza ujuza katika tasnia ya uigizaji.
Utakumbuka kuwa Gabo Zigamba ameongozana na wasanii wenzie wa filamu Tanzania kwenda Korea kwenye ziara yao ya kujifunza mambo ya filamu ambapo wana takrbani siku tatu nchini humo.
Baadhi ya mastaa wa filamu ambao wapo kwenye ziara hiyo ni Irene Paul, Wema Sepetu, Idris Sultani, Dorah, Johari Chagula, Steve Nyerere, Eliud Samwel, Getrude Mwita na Godliver Gordian.
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘10 Directory’ filamu nyingine ambazo zilichaguliwa kutoka Afrika ni kama The Painting (Zambia), Road to Kabul (Morocco), Matares (Algeria), Baby Mamas (Afrika Kusini), 10 Days in Sun City (Nigeria), O Heroi (Angola) na Photocopy ya (Misri).
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi
Leave a Reply