Shaka: Rais Samia ni turufu ya maendeleo

Shaka: Rais Samia ni turufu ya maendeleo

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amemtaja Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa turufu ya maendeleo ya Watanzania kutokana na falsafa tatu anazotumia katika uongozi wake ambazo ni upangaji, usimamiaji na utekelezaji.

Aidha, amemtaja Mkuu huyo wa nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kuwa ni mwanadiplomasia nguli wa uchumi na hilo linadhihirika kwa namna alivyopata mkopo nafuu kutoka Shirika na Fedha la Kimatafa (IMF) na namna alivyopanga matumizi yake.

Shaka aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akipokea tuzo ya kumpongeza Rais Samia kwa utendaji mzuri, iliyotolewa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema Rais Samia amekuwa turufu ya maendeleo ya watanzania kutokana na kazi kubwa anazofanya nchini kwa kuhakikisha analeta maendeleo kupitia falsafa anazozitumia.

Shaka alisema ni ukweli usiopingika katika uongozi Rais Samia kwa kipindi cha miezi tisa ambapo mambo makubwa yamefanyika."Katika kipindi hicho tumeshuhudia utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025, kwamba wanaamini kufikia mwaka 2025 utekelezaji utazidi asilimia 100,"alisema na kuongeza

"Kwa kipindi hiki kifupi cha uongozi wake, leo hii ukimsimamisha Mkuu wa Wilaya yoyote akueleze mafanikio, atatumia zaidi ya saa nane kueleza kazi kubwa imefanywa kwa muda mchache," alisema.

Alisema Rais Samia amekuwa kiongozi ambaye kila anachokikusanya anahakikisha kinakwenda katika shughuli lengwa, jambo linalothibitisha usimamizi mzuri.

Aidha, Shaka alimtaja Mkuu huyo wa nchi kuwa mwanadiplomasia nguli wa uchumi kutokana na kile alichoeleza kwamba, amefanikisha upatikanaji wa mkopo nafuu sh. trilioni 1.3 kutoka IMF na ameuelekeza katika matumizi sahihi.

Alisema fedha hizo zimeongeza mzunguko nchini na hivyo kufanya kipato cha kila mtanzania kuongezeka.

Pamoja na mambo mengine, alibainisha tuzo hiyo waliyomiabidhi Rais Samia ni ishara ya vijana kuiunga mkono wa serikali ya awamu ya sita.

Aliwataka vijana kuwa mabalozi wazuri wa Rais Samia kwa kueleza mazuri anayofanya, akiwasihi wasipofanya hivyo hakuna mtu wa nje ya nchi atatekeleza hilo badala yao.

"Mcheza kwao hutunzwa basi nanyi vijana hakikisheni mnakuwa mabalozi wazuri wa Rais wetu, ni sisi ndiyo wa kumtia moyo hakuna mwingine atakayefanya hivyo badala yetu," alisema.

Aliahidi kuandaa darasa la itikadi kwa ajili ya kuwaelimisha vijana, wafahamu nchi ilipotoka, ilipo sasa na inapoelekea.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la UDSM, Isack Sambuli, alisema tuzo hiyo waliyotoa kwa Rais Samia imetokana na utendaji mzuri aliouonyesha kwa kipindi kifupi.

Aliahidi kumtetea na kumuunga mkono wakati wote, akisema vijana hawatarudi nyuma katika hilo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags