Ni hali ya kawaida kumuona mtu anapiga miayo kwani tukio hilo hutajwa kati ya matukio yafanyikayo bila muhusika kutaka, lakini hii si kwa binadamu tu bali hutokea pia kwa wanyama kama vile, paka na mbwa.
Upigaji wa miayo watu huusisha na uchovu wa mwili, usingizi na wengine huenda mbali zaidi na kuhusisha kitendo hicho na njaa. Lakini swali ambalo watu hujiuliza ni kuhusiana na tukio hili kuwa na tabia ya kuambukizana yaani endapo mtu akipiga miayo ni rahisi sana kumuambukiza mtu wa karibu yake au mtu yeyote ambaye ataona kitendo hicho kikifanyika.
Ingawa sababu kamili ya kupiga miayo kwa kuambukiza haieleweki kikamilifu, kuna nadharia chache ambazo watafiti wamezitaja kama sababu, tafiti hizo zinaeleza kuwa uambukizwaji wa miayo hutokana na akili ya mtu kukua kikamilifu hivyo kwa watu wazima wenye afya nzuri ya akili maendeleo ya kisaikolojia yanafanya wapige miayo wakati wengine wanapiga.
Kwa tafiti za watoto ambao bado wanaendelea kukua kiakili zimegundulia kuwa wao hupiga miayo kwa uchovu tu na siyo kwa kuambukizwa, lakini pia hata kwa watu wazima mwenye matatizo ya akili hupiga miayo kwa sababu tofauti na siyo za kuambukizwa.
Pia utafiti uliofanywa na Ivan Norscia na Elisabetta Palagi wa Chuo Kikuu cha Pisa kilichopo Italy unatoa ushahidi wa kitabia kwamba uambukizi wa miayo unaweza kuwa aina ya uambukizi wa kihisia na ndiyo maana kuna uwezekano mkubwa wa kupata miayo kutoka kwa mtu unayemjali, kama vile rafiki, ndugu au mpenzi kwa sababu ya hisia ambazo akili hutengeneza.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi
Leave a Reply