Thanos Bishoo Aliyevutia Wengi Squid Game 2

Thanos Bishoo Aliyevutia Wengi Squid Game 2


Uzuri au ubaya wa sanaa ya maigizo hubebwa na stori au wahusika wanaowasilisha maudhui katika kazi hiyo. Wakati mwingine wahusika huvaa uhalisia hadi kupelekea jamii kuamini ndivyo walivyo.

Hilo limetokea katika tamthiliya ya Squid Game 2, iliyoachiwa rasmi Desemba 26, 2024 ikiwa ni baada ya kusubiriwa kwa miaka mitatu tangu ilipoachiwa sehemu ya kwanza mwaka 2021.

Katika msimu huo wa pili ameonekana muhusika mpya aliyetumia jina la Thanos, ambaye ameteka hisia za wengi kutokana na vitendo vyake vya mzaha na kutojali alivyokuwa akivionesha hata katika matukio ya hatari.

Choi Seung-hyun, ndilo jina lake halisi huku jina la umaarufu likiwa T.O.P na katika msimu huo wa pili anatambulika kama ‘Thanos’ ama mshiriki namba 230.

Katika maisha ya uhalisia nje ya Squid Game mwigizaji huyo pia ni rapper, na mtunzi wa nyimbo kutoka Korea Kusini. Amewahi kufanya kazi chini ya rekodi lebo ya YG Entertainment na alikuwa rapper mkuu katika kundi la BigBang mwaka 2006.

Kundi ambalo lilikuwa miongoni mwa makundi yanayofanya vizuri zaidi barani Asia. Hata hivyo mwaka 2010 kundi hilo liliacha kufanya kazi, lakini T.O.P akishirikiana na G-Dragon alitoa albamu iitwayo GD & TOP.

Aidha, nyimbo ambazo amewahi kuzifanya kama rapper akiwa mwenyewe 'Turn It Up' (2010) na 'Doom Dada' (2013), na zilifanikiwa kushika nafasi ya pili na ya nne kwenye Gaon Digital Chart. Mbali na kutoa kazi zake Choi Seung-hyun ameonekana katika video nyingi za muziki za Big Bang.

Katika ulimwengu wa filamu Choi Seung-hyun alianzisha uigizaji mwaka 2007 kupitia mfululizo wa vipindi vya TV kama I Am Sam (2007), kisha akaendelea na Iris (2009) filamu ya Nineteen (2009) na hata ile ya 71: Into the Fire (2010), ambapo ilifanya ashinde tuzo kadhaa.

Kati ya tuzo hizo ni Best New Actor kwenye Tuzo za Filamu za Blue Dragon za 2010 na Tuzo za Sanaa za Baeksang za 2011. Baadaye, alicheza kama muhusika mkuu katika filamu ya Commitment (2013), ikafanya ashinde tuzo ya New Asian Actor of the Year kwenye Tamasha la Filamu la Kimataifa la Busan na Tazza: The Hidden Card (2014).

Licha ya kufanya makubwa hayo katika kiwanda cha filamu Julai 2017, Choi Seung-hyun alikumbana na majanga baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 10 jela na kuzuiwa kufanya kazi ya sanaa baada ya kupatikana na hatia ya kutumia bangi, ambayo ni kinyume cha sheria nchini Korea Kusini.

Tangu wakati huo alipozuiliwa kuhusika na tasnia ya burudani ya Korea ikiwa ni takriban miaka saba ndiyo ameonekana tena kwenye Squid Game msimu wa pili. Utakumbuka kuwa muhusika huyo katika msimu wa pili akiwa na nywele zake za zambarau amecheza kama mtu kiburi asiyejali hisia za wengine, na ni mmoja wa maadui wakuu wa msimu wa pili lakini pia ni mraibu wa madawa ya kulevya.

Aidha Squid Game 3, inatarajia kuachiwa mwaka huu 2025, huku tangu kuachiwa kwake Desemba 26,2024 imeendelea kushika rekodi mbalimbali ikiwemo kupata watazamaji zaidi ya milioni 68 ndani ya siku nne.
Pia umeshika nafasi ya saba katika TV na kuwa miongoni mwa filamu maarufu huku ikipata watazamaji wengi zaidi wasiotumia lugha ya Kiingeleza.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags