Mauzauza, Ashua, Hakuna Kulala, raha na Wana ni baadhi ya nyimbo za mwanamuziki wa WCB Zuchu zilizomtambulisha kwenye gemu mwaka 2020 baada ya kutambulishwa kwenye lebo hiyo ya muziki.
Licha ya kutambulishwa miaka hiyo minne iliyopita mkali huyo nyuma alipitia msoto uliomtengenezea msingi wa kukimbiza kwenye gemu. Utakumbuka mwaka 2022 alifunguka kwenye moja ya mahojiano yake na kueleza kuwa alisota WCB kwa miaka minne kabla ya kutambulishwa rasmi.
“Mama ndio alinipeleka WCB nilipewa interview nikaimba nyimbo mbili ya kwanza ilikataliwa, ikakubaliwa ya pili ‘Wana Wana’ ndio nikachukuliwa lakini nilisugua miaka minne na kila siku nilikuwa pale unapewa nafasi ya kurekodi studio kwa Laizer unapeleka nyimbo zinasikilizwa boss anazikataa unarudi tena,” alisema Zuchu.
Lakini tunaweza kusema Zuchu hakupitia miaka minne tu kwenye msoto wa kuwa maarufu kwani ukitazama kwenye baadhi ya nyimbo za taarabu za mama yake Khadija Kopa zilizotoka miaka kumi iliyopita msanii huyo anaonekana.
Ukirudi nyuma kidogo katika wimbo ambao ulimfanya Khadija Kopa kukubalika zaidi na jamii wa ‘Full Stop’ uliotoka miaka 10 iliyopita Zuchu alikuwa ni miongoni mwa waimbaji wengine akiitikia korasi.
Hata hivyo, baada ya kumwaga wino WCB Zuchu alifanya wimbo na mama yake uitwao ‘Mauzauza’ ukiwa umetazamwa zaidi ya mara milioni 18 kupitia mtandao wa YouTube.
Zuchu na mama yake licha ya kubebana kwenye mambo mbalimbali lakini pia wawili hao wameshawahi kuchangia jukwaa moja ikiwemo kwenye zile za Kampeni za CCM.
Kwa sasa tunaweza kusema Zuchu amejipata na yupo katika ulimwengu ambao wasanii wengi wa Bongo Fleva wanatamani kufika. Na sasa anatarajia kuachia album yake ya kwanza hivi karibuni.
Leave a Reply