Msanii wa Bongo Fleva, Juma Jux kwa mara nyingine analiteka soko la muziki nchini Nigeria baada ya kushinda Tuzo ya Msanii Bora wa Afrika Mashariki kupitia tuzo za The Headies zilizotolewa usiku wa kuamkia leo Aprili 28, 2025 Jijini Lagos.
Jux kashinda tuzo hiyo ambayo alikuwa akiwania na Diamond Platnumz (Tanzania), Bien (Kenya), Bruce Melodie (Rwanda) na Azawi (Uganda).
Ukiachilia mbali Jux kushinda tuzo hiyo, pia alikuwa mmoja kati ya wasanii waliotumbuiza kwenye usiku huo, huku akiteka hisia za hadhira baada ya kuimba wimbo wake wa God Design na kucheza pamoja na mke wake Priscilla. Utakumbuka wimbo huo ni ule ambao umetikisa chart za muziki nchini humo baada ya kushika nafasi ya kwanza kupitia mtandao wa Itunes.
Katika tuzo hizo, wasanii ambao walikuwa wakiwania vipengele vingi zaidi ni Ayra Starr and Odumodublvck, kila mmoja alikuwa akiwania vipengele nane wakifuatiwa na Tems na Asake ambao kila mmoja alikuwa na vipengele sita.
Washindi wengine waliofanikiwa kunyakuwa tuzo ni London aliyeshinda tuzo ya 'Mtayarishaji Bora wa Mwaka' kupitia wimbo 'Ozeba' wa kwake Rema, ambao pia unapatikana kwenye albamu yake ya 'Heis' ya 2024. Tuzo ya 'Video Bora ya Mwaka' imechukua ngoma ya Egwu ya kwao Chike na Mohbad, ngoma iliyoongozwa na 'Director Pink'.
Wimbo Bora wa Afrobeat ni 'Big Baller' wa kwake Flavor, Msanii Bora Wa Kimataifa tuzo imeenda kwa Travis Scott kupitia wimbo wa Active aliyoshirikishwa na Asake ngoma amabayo inapatikana pia kwenye albamu ya Lungu Boy ya 2024.
Tuzo za Headies za usiku wa kuamkia leo Aprili 28, 2025 zilikuwa ni mara ya 17 tangu kuanzishwa kwake ambapo safari hii zilikuwa na vipengele 30 ambavyo vilikuwa vikiwaniwa na wasanii tofauti wa ndani na nje ya Bara la Afrika.

Leave a Reply