Mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini Diamond Platnumz ameweka wazi namna alivyofunga ndoa na msanii wake Zuchu bila kushirikisha familia yake akiwemo mama yake mzazi.
Wakati alipokuwa kwenye mahojiano na kituo cha redio cha ‘Power 105.1’Diamond, ameeleza ndoa yake na Zuchu haikupangwa na ndio maana alioa bila ya kumtaarifu mama yake mzazi.
“Naweza kusema kuwa ilikuja tu yenyewe, si kitu ambacho kilipangwa kilitokea tu. Niliamua tuu kuwa nahitaji kufanya hivi. Kwangu mimi, na kutokana na dini yangu, mambo kama haya hayatakiwi kuwa magumu au ya kuchanganya. Yanatokea tu kwa namna rahisi.
“Nilimchukuwa mke wangu tukaenda kwa Sheikh na tukafunga ndoa. Kisha nikampigia mama simu nikamwambia, “Mama, nimeoa.” Kwa hiyo, ilikuwa tu ni njia ya kawaida na ya moja kwa moja,” amesema Diamond
Hata hivyo katika mahojiano hayo ameeleza kuhusu uhusiano mzuri alionao kwa wazazi wenzake ambao amezaa nao watoto.
“Kwanza kabisa najua nina watoto, lakini pia najua kuna wengine ambao najua kuwa ni wangu, ila sitaki kubishana na mama zao na mambo kama hayo. Ninawalea wote wapo wanne hadi watano, nasema hivi kwa sababu wakati mwingine mambo yanaweza kuwa magumu, lakini ninajitahidi kwa hali na mali kuhakikisha nawalea vizuri.
“Nilienda nikafanya DNA moja pale Tanzania, na mambo yakawa magumu. Mimi niko sawa kabisa na mama wote wa watoto wangu, wananipenda, sitaki kukudanganya. Mimi ni mtu mzuri kwao. Imefikia hatua wanaume wao wengine wanakasirika wakidhani labda bado kuna kitu kinaendelea lakini hakuna chochote kinachoendelea,”amesema
Mbali na hayo ameweka wazi kuhusu uhusiano wake wa zamani na mwanamitandao maarufu Fantana ambaye walionekana kuwa karibu katika kipindi cha ‘Young, Famous & African’.
“Mimi na Fantana tulikuwa vizuri sana, tulikuwa karibu sana. Kwa hiyo unajua kwenye kile kipindi, nilikuwa kama najaribu kuonyesha watu hali halisi ya binadamu. Katika kile kipindi nilitaka kuwaonyesha watu jinsi binadamu wa kweli walivyo. Nilikuwa pale na Fantana. Sikuwa na nia ya kumdanganya, lakini ukweli ni kwamba nilikuwa namcheat.
“Kwa hiyo aliponiuliza kuhusu Zuchu nikasema huyo ni msanii wangu kwa sababu nililazimika kudanganya. Mimi na Zuchu, ndiyo tuko pamoja. Lakini wakati Fantana aliponiuliza kuhusu hilo, ningesema vipi? Unajua wakati mwingine unahitaji kutumia maneno matamu. Ukisema ndiyo, huyo ni mpenzi wangu, anaweza kukasirika,”amesema
Aidha ameongezea kwa kueleza “Ilikuwa kama vile, nisipodanganya nitampoteza. Kwa hiyo nililazimika kusema kwamba Zuchu ni msanii wangu tu. Lakini ukweli ni kwamba alianza kama msanii wangu, halafu taratibu hisia zikaanza kuibuka. Tukaingia kwenye mapenzi bila hata kutarajia, na sasa tupo vizuri sitaki kudanganya, nampenda,”amesema

Leave a Reply