Fahamu haya kuhusu Mwanamuziki Darassa

Fahamu haya kuhusu Mwanamuziki Darassa

Kwa zaidi ya miaka 10 Darassa amefanya muziki tofauti kabisa na rapa wenzake, uwezo wake wa kuchanganya vionjo na utunzi wa aina yake umefanya nyimbo zake kupendwa na watu wengi na kujizolea mashabiki lukuki.

Akiwa anafanya muziki wake chini ya Classic Music Group (CMG), Darassa ameshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), ametoa albamu moja na ni miongoni mwa wasanii Bongo wanaopata namba kubwa katika majukwaa ya kidijitali. Fahamu zaidi.

1.Darassa ambaye jina hilo alipewa na marehemu Complex, wimbo wake wa kwanza kurekodi unaitwa ‘Kieleweke’ akimshirikisha Steve RnB, na wimbo ‘Sikati Tamaa’ uliokuja kumtoa kimuziki ulikuwa ni wa pili kurekodi katika maisha yake ya muziki.

2.Watu ambao wana mchango mkubwa katika safari ya Darassa kimuziki kipindi anatoa wimbo wa kwanza ni DJ Mafuvu, Salama Jabir, DJ Steve B na B Dozen, hawa ndio walipokea CD ya kazi yake na kuipa nafasi katika redio wakati huo.

3.Tuzo ya kwanza na ya pekee kwa Darassa kushinda katika TMA ni kupitia wimbo wake ‘Loyalty’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Slave Becomes a King (2020) akiwa na Nandy na Marioo ulioshinda kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2021.

Ushindi huo ulikuja baada ya Darassa kuzibwaga nyimbo kali kama Ndombolo (Alikiba), Shikilia (Professor Jay), Unaua Vibe (Rapcha) na Lala (Jux).

4.Kuna wasanii wengi Bongo ambao Darassa amewashirikisha angalau mara mbili katika nyimbo zake, kuna Jux (Leo, Juju), Maua Sama (Shika, Tumepoteza), Rich Mavoko (Kama Utanipenda, Segedance), Ben Pol (Sikati Tamaa, Muziki) Harmonize (Yumba, Mazoea) n.k.

5.Ben Pol ndiye msanii pekee Bongo mwenye historia kubwa katika muziki wa Darassa, aliimba kiitikio cha wimbo wake, Sikati Tamaa (2012) uliomtoa kimuziki, ni ngoma iliyofanya vizuri hadi kuachia remix yake akiwa na Godzilla na Joh Makini.

Ilimchukua miaka zaidi ya mitatu kutengeneza ngoma nyingine kubwa kama hiyo, nayo ni Muziki (2016) akimshirikisha Ben Pol tena, na hadi sasa hakuna ngoma ya Darassa iliyouza zaidi katika majukwaa ya kidigitali kama hii, huku ikimpatia dili nyingi.

6.Video ya wimbo ‘Muziki’ inashikilia rekodi kama video ya msanii wa rap Bongo iliyotazamwa zaidi YouTube ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 27, ikiwa imeipita video ya wimbo wa AY, Zigo Remix akiwa na Diamond Platnumz yenye ‘views’ milioni 23.

7. Hadi sasa Marioo ndiye mwimbaji Bongo aliyeshirikishwa zaidi na Darassa, mkali huyo kutokea Bad Nation amesikika katika ngoma tatu za rapa huyo ambazo ni Chanda Chema (2019), Loyalty (2020) na News (2024).

8. Wimbo wa Darassa akimshirikisha Bien wa kundi la Sauti Sol kutoka Kenya, No Body (2023), umesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 17.6 katika mtandao wa Boomplay na ndio wimbo wa kwanza wa rapa huyo kufikia namba hizo hadi sasa.

9. Mwaka 2020 albamu ya Darassa ‘Slave Becomes a King’ ndio ilikuwa albamu iliyotoka na nyimbo nyingi zaidi kwa mwaka huo zikiwa ni 21, huku ikifuatiwa na ya Harmonize, Afro East (18) na Story of The African Mob (12) ya Navy Kenzo.

10. Darassa ndiye msanii wa kwanza Bongo kufanya kazi na Sho Madjozi kutokea Afrika Kusini ambaye amesikika katika wimbo wake maarufu, I Like It (2020) ambao video yake imetazamwa zaidi ya mara milioni 15 huko YouTube.

Baada ya Darassa ndipo wakafuata wengine kama Marioo (Mama Amina), Nandy (Kunjani) na RJ The DJ (Too Much).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags