Mwanamuziki Fareed Kubanda (Fid Q) amewapa nafasi mashabiki wake kuchagua ngoma yake ipi aimbe Mei 2, 2025 atakapopanda kwenye jukwaa la Bongo Fleva Honors.
Fid Q atafanya shoo ya saa tatu kwenye tamasha hilo ambalo msimu huu linafanyika kwenye ukumbi wa The Cask, Kawe Beach, Dar es Salaam.
Bongo Fleva Honors ni jukwaa maalumu lililoanzishwa miaka mitatu iliyopita likilenga kuwaheshimisha na kutambua mchango wa wasanii waliochonga barabara kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Baada ya wasanii mbalimbali, msimu huu ni zamu ya Fid Q kupafomu katika jukwaa hilo ambalo amesisitiza shoo yake itakuwa ya tofauti na zilizotangulia.
"Nina uzoefu wa kufanya shoo tangu mwaka 2000, wananchi wanafahamu shughuli yangu jukwaani, nitawarudisha katika albamu yangu ya kwanza ya Vina mwanzo kati na mwisho.
"Albamu yangu ya pili ya Propaganda hadi ya tatu ya kitaa Olojia, vilevile nina albamu ya nne na EP ambazo mashabiki watazisikia siku hiyo laivu," amesema.
Katika kuongeza mzuka kwa mashabiki, Fid Q amesema kabla ya shoo hiyo, mashabiki watakuwa na fursa ya kupendekeza wimbo wake upi ambao wanataka upigwe siku hiyo.
"Sitaki niwachagulie mashabiki, wao ndio wataamua kati ya nyimbo zangu nyingi, upi usikose siku hiyo," amesema.
Fid Q ambaye alitambulishwa kwenye gemu na ngoma ya Huyu na yule iliyotoka miaka ya 2000 akishirikiana na Mr Paul amesema nafasi ya kuheshimishwa kwenye Bongo Fleva Honors aliyopewa ataitendea haki.
"Nimepewa saa 3 za kufanya shoo siku hiyo, japo wengi wanafahamu Fid Q shoo nyingi anafanya kwa nusu saa hadi saa moja, hii ya saa 3 itakuwa ni zaidi ya shoo.
"Nitapafomu na rafiki zangu wa ndani na nje ya nchi ili kupata experience (uzoefu) tofauti," amesema.
Amesema wasanii ambao ameshirikiana nao kwenye ngoma zake mara kwa mara watakuwepo naye jukwaani siku hiyo.
Akizungumzia tamasha hilo na ma-legend wengine waliowahi kupafomu kwenye Bongo Fleva Honors, Fid Q amesena ana kibarua cha kuendeleza pale walipoishia watangulizi wake kwenye jukwaa hilo.
Muasisi na mwanzilishi wa jukwaa hilo, Joseph Mbilinyi (Sugu) amesema Fid Q ni miongoni mwa wakongwe walioendeleza muziki wa Bongo Fleva, hivyo anastahili heshima hiyo.
"Jukwaa hili ni kwa ajili ya mashabiki ambao walikuwa sehemu ya Bongo Fleva wakati inaanza na kukuwa, tulianza msimu wa kwanza tukiwa Upanga, msimu wa pili tulikuwa Warehouse, Masaki na misimu yote jukwaa limekuwa mafanikio.
"Msimu huu katika kutafuta viwango vya kimataifa, litafanyia The Cask, Kawe Beach na msanii tutakayekuwa naye ni Fid Q, hakuna mtu ambaye hajui mchango wake katika ukuaji na utamaduni wa Bongo Flava," amesema Sugu.

Leave a Reply