Joti afafanua kuhusu pengo lake

Joti afafanua kuhusu pengo lake

Lucas Mhavile 'Joti' ni staa mkubwa kwenye tasnia ya burudani na hasa sanaa ya vichekesho 'Komedi'. Staili zake mbalimbali za kuigiza zinawavutia wengi na kuna mambo ambayo yanawashangaza na kujiuliza maswali.

Mfano mzuri ni mwonekano wake katika meno na amekuwa akionekana katika baadhi ya video zake za komedi kwenye mitandao ya kijamii akiwa na pengo.

Wapo wanaoamini ni pengo halisi na wengine wanaamini ni ubunifu tu katika kuvutia na kutokana na lilipo ni ngumu kung'amua kama ni halisi au si halisi.

Mwananchi ilimcheki ili kupata ukweli wa swali hilo linalowaumiza wengi vichwa na mwenyewe amesema ni kweli anakutana na maswali mengi hasa kuhusu pengo hilo lakini ukweli ni anafanya tu sanaa na meno yake yute ni freshi na hayana dosari yoyote.

"Huwa nakutana sana maswali ya watu tofauti kuhusu meno yangu kama nina pengo lililooza au jeusi. Watu wanafikra tofauti na kuniona nina pengo jeusi, ila mimi meno yangu yote ni meupe peee... lile pengo jeusi linaloonekana huwa nafanya ubunifu kwa ajili ya sanaa yangu na nashukuru hii staili imewateka watu wengi sana kudhani nina pengo jeusi au lililooza,"

"Unajua kwenye sanaa, lazima uwe na ubunifu, ndiyo maana katika kujitafuta nimepitia mbinu nyingi sana ilimradi tu niweze kuwateka mashabiki zangu. Nimecheza kama mwanamke, navaa nguo za kike na kujipodoa kabisa kitu ambacho ni kigumu sana kwenye uigizaji. Uwe mwanaume halafu ujibadilishe kuwa mwanamke kwa hali yetu ya sasa, Watanzania wengi hawakuelewi ujue. Nimeigiza kama Babu Mzee, nimeigiza kama mwanafunzi, yote hii ni ubunifu wa kutaka kuwateka mashabiki na nimefanikiwa kwa hilo. Hivyo mimi sina pengo bana, leo acha niwaambie tu ukweli," alisema Joti.

Aliongeza, amekuwa akifanya hivyo kwenye mambo mengi na kabla hata ya kuamua kuigiza alijichunguza kuona kama sanaa hiyo inaweza kumpa maisha na anaiheshimu kazi hiyo hadi anazeeka.

“Mimi nilijichunguza kwa ufasaha nikajaribu kuangalia ni namna gani ninaweza kuishi ama kuendesha maisha yangu, nikaona nina kipaji cha kuchekesha ambacho kimenipa umaarufu mkubwa,” alisema.

“Nimeshaamua kuzeekea kwenye uchekeshaji kwani umenisaidia kuwa na maisha mazuri, kwa hiyo ni lazima niheshimu fani hii ambayo imeniweka mjini.”






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags