Kina Dada Na Dunia Ya Michezo Ya Hela

Kina Dada Na Dunia Ya Michezo Ya Hela

Sisi wengine ni wajanja. Tunajua namna ya kuishi kwa akili na hawa viumbe. Ni agizo la 'Saa Godi' kwa sisi wanaume wote duniani. Ya kwamba tuishi kwa akili na hawa viumbe uzao wa Eva. Bila hivyo dunia itakuwa kitu kigumu kwetu.

Na kwa ujanja huo huo. Tunajua ya kwamba simu za ‘madem’ za saa 12 jioni hadi saa 2 usiku. Hazifai kabisa kupokelewa. Siyo mahaba wala huba, hilo ni pira la moto. Usipokee kaka. Hapo hutafutwi wewe inatafutwa hela ya mchezo. Ndiyo mida yao hiyo.

Imekuwa kama 'fasheni' sasa. Kila pisi kali inacheza mchezo wa hela mtaani kwao. Ni kama walikutana tena na 'bebi nyoka' wao. Akawapa akili mpya ya kutufanya 'wababa' tuendelee kuvujishwa jasho. Maana hizo pesa zenyewe zinatoka kwetu.

Ukikaa baa utaona wahudumu wanafuatwa na mwanadada wa nje ya ofisi. Anakusanya pesa kwa wahudumu mmoja kwa mmoja. Mimi mwanzo nikajua ni utaratibu wa baa za Kimara tu. Kumbe ni kila sehemu na kila ofisi kuna hizi mishe. Wadada wako bize.

Kwenye maofisi hivyo hivyo. Mpaka watoto wa hosteli za vyuo vingi wana michezo yao. Hata wale waliogeuza miili yao kuwa 'fremu' za biashara ya ngono. Na wao maeneo yao ya kujidai wana michezo ya pesa. Kimsingi ni dili kubwa kikeni.

Yaani anaenda kufungua 'fremu' yake mida ya usiku. Hata mchana kwa wanaotumia mitandao kurahisisha huduma. Wakipata kiasi kutoka kwa wanaume wapenda ngono. Anapeleka kwanza hela ya mchezo, kisha anarudi kwenye 'fremu' yake kuendelea na biashara.

Sasa hawa wa majumbani ambao wengi wao ni wake za watu. Hawa ndiyo wana kitu cha pekee sana. Wengi wao wakipata hela ya mchezo siku ya kupokea. Hao kiguu na njia kwenda kumtunza shoga'ake harusini au kwa shughuli yoyote tu. Wadada wako na dunia yao.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags