Kumbe Appy na Baddest ilikuwa hivi..

Kumbe Appy na Baddest ilikuwa hivi..

Ni wazi kuwa mwanamuziki Appy ni kati ya waliofanya vizuri kwa mwaka 2024 kutokana na kazi zao walizoachia. Kati ya nyimbo alizotoa msanii huyo ni 'Marry Jane' iliyotoka Desemba 11, 2024 akimshirikisha msanii wa miondoko ya reggae na Dance Hall, Baddest 47.

Akizungumza na Mwananchi Scoop Appy ameeleza namna ambavyo haikuwa ngumu kwake kupata kolabo na Baddest.

"Alivyoona nimeweka kipande cha wimbo huo kwenye mitandao yangu ya kijamii, alipenda idea akaomba kushiriki na kiukweli ukiangalia kwa upande wa Dance hall kwa hapa nyumbani huwezi muacha Baddest. Sikujiuliza maswali mara mbili kwa sababu alistahili kuwepo kwenye kazi hiyo, "amesema

Amesema wimbo huo umetengeneza mafanikio yaliyopelekea atafutwe na msanii mwenye asili ya Jamaica anayeishi Marekani ambaye pia amependa kuufanyia remix.

"Kwa bahati nzuri tumepata tena Mjamaica ambaye yupo Marekani amependa huo wimbo na ameingia na tutatoa remix," amesema Appy.

Appy ambaye dunia ya muziki ilimtambua vizuri kupitia wimbo wake wa ‘Watu Feki’ ameongezea kuwa anajivunia aina yake ya uimbaji.

"Utofauti na meseji ya wimbo huo ambao kila mtu alipenda. Hauwezi ukatembea mahali ukauliza 'Watu Feki' watu wasiujue. Meseji yake pia ilikuwa noma kwa sababu watu wengi wanapitia mambo mengi na wanapambana kutoka sahemu mmoja kwenda nyingine," amesema Appy.

Appy amekuwa akisifika kwa mtindo wake wa uimbaji ukiwekwa katika levo za kimataifa amesema ni vyema mashabiki wakapenda vya kwao kwanza.

"Mimi naamini wasanii kama Tems na Ayrra Star wanamashabiki wengi kutokea Afrika Mashariki lakini unakuta ni ngumu msanii anayetokea nyumbani kupewa sapoti. Imekuwa kitu kigumu sana kwa watu wengi kuangalia nyumbani mimi nafikiria tuwaangalie wasanii wa nyumbani kwa jicho la tatu.

"Tuangalie kwanza tuna nini nyumbani tukifahamu na sisi siku moja tunaweza kupata Grammy na matuzo makubwa. Anaweza asiwe Appy labda akawa ni msanii aliyekuwa inspired na Appy kikubwa ni kufanya muziki mzuri kwa ajili ya nchi yetu," amesema Appy.

Appy ameongezea kuwa lebo inayomsimamia inaweza kumfikisha mbali na ndio maana hata nyimbo zake nyingi hutayarishwa na prodyuza Ibra Jacko ambaye ndio mmiliki wa lebo hiyo.

"Yeah nafanya kazi na Magical Touch ambayo C.E.O ni Ibra Jacko ambapo watu wengi wanauliza mbona nafanya nyimbo zangu sehemu moja kwa sababu na mkataba nao kabisa.

" Mimi naamini kwenye muziki mzuri kama lebo inanisaidia kupata good music sina shaka nao kabisa kwa sababu ndio kitu kitanifikisha mbali zaidi. Tofauti na mambo mengine ninachoweza kusema wao ni sehemu ya kunipa muziki mzuri," amesema Appy.

Licha ya muda wake mfupi katika tasnia muziki Appy amefanikiwa kupata collabo kubwa kutoka kwa wasanii wa Hip-hop akiwemo Lunya, Stamina, Roma, Izzo Bizzness na wengine wengi.

"Ni wasanii wakubwa ambao nimepata nafasi ya kufanya nao collabo kama Roma ambaye ni nguli kabisa siwezi kuchukulia poa. Mtu kama Stamina, Lunya na wengine ni mafanikio makubwa sana na siwezi kuchukulia kwa udogo ni alama wameacha kwenye muziki wangu," amesema Appy.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags