Kwa Mara Ya Tano, Diddy Akataliwa Dhamana

Kwa Mara Ya Tano, Diddy Akataliwa Dhamana

Jaji wa shirikisho Arun Subramanian amekataa ombi la dhamana la Sean "Diddy" Combs katika uamuzi mpya uliotolewa mapema jana Jumatatu, Agosti 4,2025.

Hii inakuwa mara ya tano kwa Combs, kukataliwa kutoka katika gereza hatari zaidi jijini New York liitwalo ‘Metropolitan cha Brooklyn’. Ambako amekuwa akishikiliwa tangu Septemba 2024.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakamani zilizopatikana na jarida la People, jaji Arun aliandika kuwa mahakama lazima ijiridhishe kwa usahidi wa wazi ili kumuachia rapa huyo.

“Lazima mahakama ijiridhishe kwa ushahidi wa wazi na wa kushawishi kwamba mtuhumiwa hana uwezekano wa kutoroka wala si tishio kwa usalama wa mtu yeyote au jamii endapo ataachiwa huru. Combs anaonekana kuwa ni hatari hivyo anaweza kutoroka au kuhatarisha wengine,” amesema Arun Subramanian

Jaji aliendelea kueleza kuhusu masharti ambayo yanatakiwa ili Combs aachiliwe “Sababu za kipekee zinazostahili kuachiliwa huru, pale ambapo hakuna ubishi kuwa mshtakiwa si tishio la kutoroka wala hatari.

"Na ambapo mazingira ya kipekee yanatoa msukumo wa kuachiliwa, yakiwemo umri mkubwa wa mshtakiwa na matatizo makubwa ya kiafya yanayohitaji matibabu ambayo huenda kituo cha MDC kisiweze kutoa. Hivyo nimeshindwa kudhibiti kama anastaili kuachiwa kwa dhamana,” amemalizia jaji Arun

Uamuzi huo umetolewa siku chache baada ya mpenzi wa zamani wa Combs, Virginia "Gina" Huynh ambaye alikuwa muhusika wa tatu kutoa ushahidi katika kesi ya rapa huyo kuandika barua akiomba Combs aachiwe kwa dhamana.

Katika barua yake, Huynh ambaye alijitambulisha jina lake halisi kwa mara ya kwanza alimuomba Jaji Subramanian ampe Combs dhamana ili akaendelea kuwatunza watoto na familia yake. Pia kuendelea na majukumu yake huku akiwa chini ya uangalizi wa mahakama.

Utakumbuka Julai 28,2025 mawakili wa Combs waliwasilisha ombi la kutaka mteja wao aachiwe kwa dhamana ya dola milioni 50 pamoja na dhamana ya nyumba yake iliyopo Miam huku akisubiri hukumu yake inayotarajiwa kutolewa Oktoba 3,2025.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags