Mastaa Wengine Watajwa Kesi Ya Diddy

Mastaa Wengine Watajwa Kesi Ya Diddy

Aliyekuwa msaidizi wa Diddy, Mia ameendelea kusimama kizimbani ikiwa ni siku yake ya tatu mfululizo. Wakati wa uwasilishwaji wa ushahidi amewataja mastaa wengine watano katika kesi hiyo ambao hawakutolewa ufafanuzi zaidi.

Mia aliwataja mastaa wakubwa katika mazungumzo yake baada ya kuoneshwa ujumbe aliowahi kumtumia Diddy ambapo alimtaja Mick Jagger, Leonardo DiCaprio, Jennifer Lopez (J.Lo), Chadwick Boseman huku kukiwa hakuna maelezo zaidi kuhusiana na mastaa hao kutajwa katika kesi hiyo.

Hata hivyo wakati alipoulizwa swali na wakili wa Diddy, Brian Steel kuhisiana na ujumbe aliomtumia Combs mwaka 2019 ambapo katika ujumbe huo Mia alimweleza Combs jinsi alivyomwokoa kwenye ndoto mbaya ambayo alikuwa amekwama kwenye lifti na R. Kelly.

Mbali na hilo pia Mia aliambiwa asome ujumbe mwingine aliomtumia Diddy Agosti 29,2020 ambapo alituma ujumbe akikumbuka matukio ya furaha katika miaka minne ya kufanya kazi kama kunywa champagne kwenye Mnara wa Eiffel saa kumi alfajiri pamoja na Diddy kukataa ombi la msanii Mick Jagger kuondoka na mfanyakazi huyo.

Aidha mwanadada huyo alieleza kuwa kipindi chote alipokuwa akituma jumbe hizo alikuwa bado hajajitambua kisaikolojia huku akisisitiza kuwa hajaidanganya mahakama na kuwa amezungumza ukweli mtupu.

“Sijawahi kusema uongo mahakamani hapa, na sitawahi kusema uongo. Kila kitu nilichosema ni kweli. Imekuwa safari ndefu. Najaribu kufumbua mambo. Nipo kwenye tiba ya kisaikolojia,”amesema Mia

Utakumbuka katika ushahidi wake aliotoa mahakamani wiki iliyopita Mia, aliyekuwa msaidizi wa zamani wa Diddy alieleza kuwa msanii huyo alimnyanyasa kingono kwa nyakati tofauti huku akimlazimisha kumbusu na kutaka kufanya naye ngono katika sherehe ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa ya miaka 40.

Mpaka kufikia jana (Jumatatu), watu wawili muhimu wa upande wa mashtaka tayari walikuwa wamesimama kizimbani kutoa ushahidi katika kesi hiyo akiwemo aliyekuwa mpenzi wa Diddy. Cassie (Casandra Ventura), Mia huku shahidi mwingine wa tatu anayejulikana kama Jane anatarajiwa kusimama kizimbani wiki hii, kama sehemu ya mashahidi wakuu wa upande wa mashtaka.

Diddy, mwenye umri wa miaka 55, atakabiliwa na kifungo cha maisha gerezani endapo atapatikana na hatia katika mashtaka ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, uhalifu wa kupanga na mashtaka mengine. Lakini rapa huyo amekana mashtaka yote dhidi yake.

Utakumbuka Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan huko Brooklyn.

Kabla ya kukamatwa kwa Diddy, Machi 25,2024 nyumba zake mbili ya Los Angeles na ya Miami zilifanyiwa upekuzi na maafisa wa usalama wa Marekani ambapo wakati wa upekuzi huo walikuta vitu kama Bunduki zisizo na usajili, dawa za kulevya, mafuta pamoja na vilainishi zaidi ya 1000.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags