Neno Msanii wangu inavyowaponza wasanii wenye lebo

Neno Msanii wangu inavyowaponza wasanii wenye lebo

Wapo baadhi ya wasanii Bongo ambao wamewahi kutambulisha wasanii kupitia lebo zao. Mwishoni mwa 2024 Omary Ally maarufu kama Marioo alimtangaza ‘msanii wake’ wa kwanza aliyemsajili kwenye lebo yake ya BadNation anayeitwa Stans.
Lakini Marioo sio msanii wa kwanza kuanzisha lebo na kusajili wasanii. Trendi hii ya wasanii kuanzisha lebo ilianza 2015 na kuna orodha ndefu ya wasanii na lebo zao.
Mwaka 2020 Shilole alitangaza kuanzisha lebo ya muziki inayoitwa Shishi Gang. Siku anatangaza lebo hiyo kwa mara ya kwanza ilikuwa pia ni siku ambayo alimtangaza ‘msanii wake’ anayeitwa Renzo.
Mpaka hivi tunavyozungumza Renzo siyo msanii wa Shishi Gang tena, lakini Shishi Gang bado ipo na 2023 ilitambulisha msanii mpya anayeitwa Nice. Unawajua Renzo au Nice?
Mwaka 2016, Ommy Dimpoz alianzisha lebo yake ya muziki ya kuitwa PKP na alimtambulisha msanii anayeitwa Nedy Music. Sina uhakika kama PKP bado ipo, lakini ambacho nina uhakika nacho ni kwamba Neddy siyo msanii wa Ommy Dimpoz tena. Unazijua ngoma ngapi za Neddy?
Mwaka 2020 rapa Joh Makini alizindua lebo yake na kuipa jina la Makini Records. Wakati anazindua pia alimtambulisha ‘msanii wake’ anayeitwa Ottuc William, lakini kwa mujibu wa Instagram ya Ottuck haionyeshi kama bado ni msanii wa Joh Makini. Unajua Ottuck anaimba muziki wa aina gani?
Alipotoka WCB, Harmonize alianzisha lebo yake ya Konde Gang, kisha akamsajili Ibraah na baadaye akaongeza wasanii wengine akiwemo Country Boy pamoja na kuwavuta wasanii waliokuwa wanafanya kazi Kings Record ya Alikiba, Cheedy na Killy.
Mpaka dakika hii ni msanii mmoja tu aliyebaki Konde Gang kati ya wanne waliokuwapo. Amebaki Ibraah peke yake. Lini ni mara yako ya mwisho kumsikia Cheedy na Killy?
Mwaka 2021 Rayvanny alizindua lebo yake inayoitwa Next Level Music na pia alitambulisha ‘msanii wake’ anayeitwa MacVoice. Habari nzuri ni kwamba Macvoice bado yuko Next Level. Unaijua ngoma ya mwisho ya MacVoice inaitwaje?
Mwaka 2015 Diamond Platnumz alimtambulisha msanii anayeitwa Harmonize kupitia lebo yake ya WCB. Baadaye akamuongeza Rayvanny, kisha Lavalava, Rich Mavoko, Queen Dareen, Mbosso, Zuchu na D Voice. Kwa sasa Rich Mavoko, Rayvanny na Harmonize na Mbosso walishatoka lakini bila shaka unafahamu walipo wasanii hao na wanachofanya.
Maswali niliyouliza hapo juu yalikuwa na lengo la kuchochea fikra zako kuhusiana na jinsi wasanii wa Bongo wanavyoanzisha lebo. Je wanaanzisha kwa sababu ni kitu wanachoweza kufanya au wanaanzisha kwa sababu wanajisikia raha kusimama mbele za watu na kusema neno ‘msanii wangu’
Na nitabisha mpaka asubuhi ikitokea mtu akisema wanaanzisha kwa sababu wanaweza. Mimi naamini hawawezi na hoja yangu inabebwa na takwimu.
Takwimu zinaonyesha asilimia 90 ya lebo zote zilizoanzishwa na wasanii zimeishia topeni. Wasanii wao hawajafanya vizuri mtaani na walipotoka kwenye hizo lebo ndo wameishia kusikojulikana. Na kama huamini, jaribu kujibu kila swali nililouliza hapo juu uone utapatia mangapi.
Wasanii wengi wanapofungua lebo wanasema lengo ni kuwashika mkono wasanii wengine kama ambavyo wao walishikwa mkono. Ukweli ni kwamba kumshika mkono msanii mwenzako siyo lazima iwe kupitia kumsajili kwenye lebo na kumuita ‘msanii wako’.

Msanii anaweza kumsaidia msanii mwenzake kwa kumpa kobalo bure au kwa malipo kidogo, kumtambulisha kwa wadau wa muziki kama vile wasanii wengine, maprodyuza maarufu, Madj, watengeneza video, waandaa matamasha na kadhalika.
Kwa kifupi wasanii wana lengo zuri, lakini kutamani kusema neno ‘msanii wangu’ ndiyo kunawaponza.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags