Nuh Mziwanda, Harmonize walivyoyageuza mapenzi fursa

Nuh Mziwanda, Harmonize walivyoyageuza mapenzi fursa

Licha ya muziki wake kutaliwa na drama nyingi kutokana na kuwa na uhusiano na Shilole kipindi cha nyuma, hiyo haiondoi ukweli kwamba Nuh Mziwanda ni miongoni mwa wasanii wa Bongofleva wenye talanta kubwa.

Kwa miaka yake zaidi 10 ndani ya muziki tayari ameandika kitabu chake cha historia kwa yale aliyoyakamilisha hadi sasa, Nuh ametoa nyimbo kubwa, kuanzisha rekodi lebo huku akiwa na EP moja mkononi. Mfahamu zaidi.

Ukiachana na kuimba na kucheza, pia Nuh Mziwanda ni mtayarisha muziki akitengeneza nyimbo zake nyingi na za wasanii wengine wa Bongofleva kama Moni Centrozone, Mr. Kesho, Alikiba, Matonya n.k.

Kutokana na kujua kutayarisha muziki, mwaka 2017 Nuh Mziwanda alianzisha lebo yake, Last Born Records ambayo jina lake linatokana na yeye kuwa mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yao ingawa hadi sasa hajamsaini msanii yeyote.

Tangu kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Shilole, Nuh Mziwanda ametoa nyimbo tatu zikizungumzia mapenzi yao yalivyokuwa na kile anachotaka sasa, nyimbo hizo ni Jike Shupa (2016), Mama Ntilie (2020) na She Roll It (2021).

Hiyo ni sawa na Harmonize ambaye katika uhusiano, kuachana na kurudiana na Kajala, alimtungia nyimbo sita ambazo ni Ushamba (2020), Vibaya (2021), Mtaje (2021), You (2022), Deka (2022) na Nitaubeba (2022).

Nuh Mziwanda ni miongoni mwa wasanii wa Bongofleva ambao wamewahi kutoa nyimbo za Injili baada  ya kuachia, Moyo Wami (2024). Wengine ni Harmonize (Omoyo), Nandy (Wanibariki EP), Linex (My Side B EP) na Mimi Mars (Christmas with Mimi Mars EP).

Kwa miaka 11 ndani ya Bongofleva, Nuh Mziwanda hajafanikiwa kushinda tuzo wala kutoa albamu ila ana Extended Play (EP) moja, Wonders (2022) iliyotoka na nyimbo sita akiwashirikisha Young Lunya, Billnas, Maua Sama, Mayunga na Vanillah.

Urafiki na ukaribu wa kikazi kati ya Nuh Mziwanda na Alikiba ulianza tangu wakiwa vijana wadogo kutokana baba zao walikuwa wanafanya kazi sehemu moja miaka ya nyuma.

Kipindi ana uhusiano na Shilole waliunda kundi lao ‘Shiwonder’ ikiwa ni muunganiko wa majina yao, waliotoa wimbo mmoja tu, Ganda la Ndizi (2015) ambao ulikuja baada ya kuwepo tuhuma za kuwa Nuh analelewa na Shilole.

Couple nyingine Bongo zilizotoa nyimbo kisha kuachana ni Diamond Platnumz na Tanasha Donna (Gere), Vanessa Mdee na Jux (Juu & Sumaku), Lord Eyes na Ray C (Kwa Ajili Yako), Lady Jaydee na Spicy Music (Together Remix). 

Wengine ni Izzo Bizness na Abela (Dangerous Boy, Umeniweza & Tumeoana), One The Incredible na Grace Matata (Salamu & Light It Up), Amini  na Linah (Mtima Wangu), Kusah na Ruby (Kelele, Chelewa & Nandondosha) n.k.

Baada ya Nuh Mziwanda kuachia wimbo wa Jike Shupa (2016) akimshirikisha Alikiba na kupata mapokezi mazuri, alifanya shoo nyingi kuliko wakati wowote ule kiasi cha kupata fedha nyingi hadi kujenga nyumba yake.

Hiyo ni sawa na Whozu, dansa wa zamani ambaye alinunua gari lake la kwanza baada ya wimbo wake wenye vituko vingi, Huendi Mbinguni (2018) kumpatia shoo nyingi nchini, sehemu ya fedha alizopata ndipo akanunua gari aina ya Crown.

Ikumbukwe Whozu alipata umaarufu zaidi Instagram baada ya Diamond kuposti video yake akicheza kwa kuchekesha wimbo, Rockonolo (2017) aliyoshirikiana na Lumino, Mohombi na Franko. Na tangu hapo wasanii wakaanza kumuomba awe anacheza nyimbo zao.

Na Peter Akaro






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags