Chatu Mandota Awachana Wanaosema Hajui Kuigiza

Chatu Mandota Awachana Wanaosema Hajui Kuigiza

Mwigizaji na mchekeshaji kutoka nchini Chatu Mandota ambaye kwa sasa anashiriki kwenye tamthilia mpya ya Vacation inayoongozwa na Jacob Steven ‘JB’ amewataka baadhi ya mashabiki wanaomnanga hajui kuigiza wampe muda kwani ndio anajitafuta.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu ameomba mashabiki wampe muda kama ambavyo walimpa kipindi anaanza uchekeshaji.

"Mimi naomba waendelee kunipa muda kwa sababu hata nilipoanza kwenye komedi hawakunipokea moja kwa moja, lakini niliendelea kufanya mpaka wakakubali kijana anajua kwahiyo wanipe muda, najua wapo na hizo komenti zipo nyingi kwa sababu mimi sio nabii kwamba chochote nachofanya kikubalike moja kwa moja hapana, kwahiyo nachowaomba wanipe muda tu," amesema Mandota.



Safari yake ya uigizaji ilipoanzia…
"Mimi nilianza sanaa mwaka 2009 huko Gongo la Mboto kwenye vikundi vya hapa na pale, baadaye nikawa nafanya komedi lakini ndoto yangu mimi ilikuwa ni kufanya filamu siriasi watu hawawezi kukupa kazi kama hawajakuona unafanya nini, kwa hiyo nilikuwa nafanya ikitokea vimeo napiga nimeshacheza kwenye Saluni ya Mama Kimbo nikacheza kama mganga," amesema Mandota.

Alivyokataliwa mara mbili kushiriki kwenye ‘Vacation’
“Ilivyotokeaga mchongo wa Vacation kuna mtu alinipigia akaniambia kuna Tamthilia JB anaianzisha inaitwa Vacation, nikaenda kwenye usahili lakini bahati mbaya sikupita, lakini ikaja swala la script watu wengi waliyopewa script walifeli nikaitwa lakini bado sikupita kuna chaguo lao tayari lilikuwepo, wakaanza kufanya na hilo chaguo lao lakini likawaangusha hakupafomu kile kitu ambacho wao wanataka nikapigiwa tena mimi simu.

“Walikuwa wameshaingia hadi kambi nikaenda nikakutana na JB akaniambia watu wanakupambania sana sijui kwanini labda una kitu cha tofauti embu nioneshe, nikafanya mazoezi kwa script aliyoshindwa yule jamaa nikafanyia mazoezi siku hiyo hiyo nikapafomu pale walishangaa sana, basi mzee akakubali na kunipa mkataba nikapewa script zote mpaka sasa napafomu," amesema Mandota.

Aidha ameeleza kuwa Vacation inakuwa filamu yake ya tatu aliyocheza akiwa ‘Serious’ na pia ni kazi yake ya kwanza aliyocheza kama mmoja wa wahusika wakubwa.
“Hii inakuwa filamu yangu ya tatu ya ‘Serious’ tofauti na komedi, ya kwanza nilicheza na Jplus, nikacheza Saloon ya Mama Kimbo, na hii ya Vacation ambayo ndio nimecheza kama moja ya wahusika wa kubwa" amesema Mandota.

Chatu Mandota ambaye anacheza kwenye tamthilia ya Vacation, kama Isco amesema uhusika wake katika filamu hiyo ni wakitofauti ukilinganisha na wahusika wengine.

“Mimi humo nimecheza kama Isco, kijana ambaye nina akili sana tofauti na vijana wote waliyopo mule ndani yaani mimi nipo hatua mbili mbele yao najua vitu vingi kuliko wao, sio mropokaji kama wengine ndio maana hata JB alikuwa ananielewa ukiangalia sehemu ya mwisho JB alitoa ofa ya watu kutoka lakini mimi pekeangu ndio nilijua kile kitu kwa sababu watoto wote hawakuwepo kwa sababu hawatumii akili," amesema Mandota.

Hata hivyo, ameweka wazi licha ya kupenda kufaya filamu za serious haitomfanya kuacha komedi na badala yake atafanya vyote.

“Mimi nitakuwa napiga miguu yote kama Ronaldo napiga kushoto, napiga kulia, kama mwanamuziki tu utakuta anaimba Amapiano, Singeli, Mduara, Bongo Fleva kwa hiyo na mimi komedi nafanya na siriasi nafanya kwa sababu zote zinanipa pesa na zinaniheshimisha, komedi naendelea kufanya kwasababu na mashabiki zangu tayari huko na siriasi ndio natengeneza mashabiki wapya," amesema Mandota.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags