Msanii wa muziki wa Singeli ambaye pia ni Dj wa kimataifa, Dj Travella ameweka wazi safari yake ya mafanikio katika muziki huo mpaka kupata nafasi ya kwenda kufanya shoo kimataifa.
Akizungumza na Mwananchiscoop, Travella amesema harakati za muziki wa Singeli alianza kitambo lakini tobo la kwenda kimataifa alilipata mwaka 2022 ambapo nchi ya kwanza kwenda kufanya shoo ilikuwa Hispania katika mji wa Barcelona.
"Nilianza mwaka 2022 kwenda nje ya Tanzania kufanya shoo na nchi yangu ya kwanza kwenda ilikuwa Hispania katika mji wa Barcelona kwenye Tamasha la Primavella Sound," amesema.
Amesema mchongo huo alipewa na Meneja wa wasanii wa Singeli Kimataifa, Abbas Jazza ambaye walisaini naye mikataba na mpaka sasa wanafanya kazi pamoja.
"Connection kuna kaka yetu anaitwa Abbas Jazza, yeye ndiye huwa anachukua wasanii, anawatafutia shoo nchi za nje kisha anawapeleka, kwahiyo mimi nilimtafuta huyo tukaelewana na kusaini mikataba akanipeleka na kweli nimeendelea kufanya shoo mpaka sasa," amesema Travella.
Amesema mapokezi ya muziki wa Singeli Kimataifa ni mkubwa kwani wasanii wa nchi hizo wanatamani kufanya kazi kwa kuchanganya muziki wao na Singeli.
"Mapokezi ni mazuri na hata wasanii wa huko wanatamani kufanya kazi na wasanii wa Bongo kuanzia waimbaji mpaka Ma-Dj wanapenda tuchanganye miziki yao na yetu ili tufanye kitu," amesema.
Amesema licha ya kuwepo kwa saundi nyingi duniani lakini muziki wa Singeli umekuwa na ushindani mkubwa kimataifa kutokana na kasi ya biti zake.
"Ushindani ni mzuri kwa sababu Singeli tunajivunia muziki wetu unakimbia, una vitu fulani vyenye vaibu, yaani muziki wa Singeli hata inapopigwa Amapiano watu wamechoka lakini inapoingia Singeli wanaamka tena."
Amesema bado inakuwa ngumu kwa wasanii na Ma-Dj wa muziki huo kupata shoo za nje kutokana na viongozi wanaowasimamia bado hawajatilia mkazo kutafuta nafasi za kupafomu nchi za nje.
"Kwa wasanii na Dj inakuwa ngumu kupata shoo za nje kutokana na Management zinakuwa hazijajikita kutafuta shoo za nje, wengi akili imelemaa Bongo, ndio maana inakuwa ngumu kwa upande wao kwenda nje, lakini kwa mtu anayenisimamia hafanyi kazi Bongo ila anafanya kazi kuwatafutia wasanii shoo nje ndiyo maana tunasogea," amesema Travella.
Aidha, kwa upande wake meneja wa wasanii wa Singeli nchini, Masudi Bashiri Kandoro 'Meneja Kandoro' amesema ni kweli wasanii na viongozi wanaowasimamia bado hawalijui vizuri soko la muziki huo kimataifa vizuri.
"Ni kweli wasanii na menejimenti zao zinazowasimamia bado hawana uwezo mzuri wa kufanya muziki huu kibiashara, bado hawajajua wanataka kufanya nini, nachoweza kuwaambia ni kwamba umeneja ni taaluma kama taaluma nyingine, wajitahidi wapate ujuzi.
"Sio lazima waende shule, kuna kozi ndogo za kufanya uelewe biashara ya muziki inaendaje, muziki utakuwa wa dunia, kesho utakutana na Meneja wa Wizkid, Tyla, Chriss Brown mtafanya biashara kwa namna gani, wasidhani wataenda Morogoro kila siku," amesema.
Amesema wasanii wengi wa singeli hawajui lugha nyingine tofauti na Kiswahili kitu ambacho kinapelekea wapishane na fursa nyingi za mafanikio Kimataifa.
"Moja ya eneo baya sana inayotupa changamoto ni lugha, unakuta msanii ni mkubwa na anatamanai kufanya kitu na msanii wetu lakini hapa katikati wanashindwa kuelewana, kwahiyo wasanii wetu wanapoteza fursa nyingi kwa kushindwa kujiendeleza, tumeona Harmonize, Diamond, Rayvanny walikuwa hawawezi kuzungumza Kingereza lakini leo ni watu wanazungumza, Kingereza ni lugha ya biashara duniani kwa hiyo watu lazima wakubali," amesema.
Hatahivyo, Kandoro amesema tayari wameshatuma maombi kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni 'UNESCO' kwa ajili ya kuwa na siku maalum ya muziki wa Singeli duniani.
"Sasa hivi tupo kwenye harakati ya kufanya huu muziki utambulike kama urithi usioshikika, tumekuwa na vikao na UNESCO na tumewasilisha maombi yakipita tutakuwa na siku ya Singeli Duniani," amesema Kandoro.

Leave a Reply