Mahakama ya juu nchini Marekani imekataa kusikiliza kesi iliyodai kwamba wimbo wa Ed Sheeran kutokea Uingereza, Thinking Out Loud (2014) umekiuka haki miliki ya wimbo wa Marvin Gaye, Let’s Get It On (1973).
Jumatatu hii mlalamikaji aliomba majaji kuisikiliza kesi hiyo ya muda mrefu ila ombi hilo lilikataliwa ikiwa ni baada ya mahakama ya chini kutupilia mbali kesi hiyo hapo Novemba kwa kusema nyimbo hizo zinafanana katika misingi ya kawaida ya muziki.
Ikumbukukwe Sheeran aliyevuma zaidi na kibao chake, Shape of You (2017), amekumbwa na kesi kadhaa kuhusu wimbo huo (Thinking Out Loud) ambao ulishika nafasi ya pili kwenye chati ya Billboard Hot 100 na kudumu kwenye chati hiyo kwa wiki 58.
Kesi hiyo dhidi ya Sheeran ilifunguliwa mwaka 2017 na kampuni ya Structured Asset Sales inayomilikiwa na mwekezaji David Pullman, ambayo inamiliki sehemu ya haki za wimbo huo wa Marvin Gaye, mwanamuziki kutokea Marekani.
Structured Asset Sales iliwashtaki Sheeran, lebo yake ya muziki ya Warner Music na kampuni ya usambazaji wa muziki ya Sony Music Publishing, ikidai fidia ya fedha kutokana na madai ya kufanana kwa nyimbo hizo mbili.
Baada ya uamuzi huo wa mahakama, mwandishi mwenza wa wimbo ‘Thinking Out Loud’, Amy Wadge, mnamo Jumanne hii, Juni 17 aliiambia BBC kuwa uamuzi huo ulikuwa ni ahueni kubwa kwake.
“Kwa kweli kabisa, wimbo huo ulibadilisha maisha yangu. Sikuwa na wimbo maarufu hadi nilipofikisha miaka 37, na huo ndio uliokuwa wa kwanza. Nilihisi kuwa nimefanikiwa, lakini ghafla hali ikabadilika, hali ilikuwa ya kutisha sana,” alisema Wadge.
Ikumbukwe Novemba 2024, jaji wa mahakama ya rufaa aliamua kwamba Sheeran hakukiuka haki miliki ikisema nyimbo hizo zinafanana msingi ya muziki ambao hauwezi kumilikiwa na mtunzi mmoja tu, na hivyo ikatupilia mbali kesi ya Structured Asset Sales.
Wimbo ‘Thinking Out Loud’ kutoka katika albamu ya pili ya Ed Sheeran, X (2014), kwa mara ya kwanza ndio ulimwezesha kushinda tuzo mbili za Grammy 2016 kama Wimbo Bora wa Mwaka na Mtumbuizaji Bora wa Pop.
Katika dokumentari ya Disney+, The Sum of It All 2023, Sheeran alisema ataacha muziki ikiwa itathibitiki alinakili wimbo huo wa Marvine Gaye kama inavyodaiwa na warithi wa mwandishi mwenza, Ed Townsend ambao walishirikiana na Structured Asset Sales kufungua kesi.
Mwaka 2017, warithi wa Ed Townsend walifungua kesi ya awali, ikiongozwa na binti yake na mrithi wa pekee, Kathryn Griffin Townsend ila kesi hiyo ikafufuliwa tena na kumalizika Mei 2023 na Sheeran hakuonekana na hatia lakini walalamikaji wakarejea tena mahakamani.

Leave a Reply