G Nako autumikisha muziki anavyotaka

G Nako autumikisha muziki anavyotaka

Awali lilipotajwa jina G Nako, wengi kwenye vichwa vyao zilisikika ngoza za hip-hop, lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwani msanii huyu ameendelea kuonesha uwezo wake wa kutambaa na midondoko ya aina tofauti tofauti ya muziki.

Kwa mara ya kwanza msanii huyo alifahamika kupitia kundi la Hip-Hop la Nako 2 Nako kundi ambalo lilikuwa linaundwa na wanachama wanne ambao ni Lord Eyez, G Nako, Ibra da Hustler na Bou Nako. Msanii Ibra Da Hustler alijitoa kwenye kundi Novemba, 2008.

Baadhi ya nyimbo maarufu walizotoa ni pamoja na Ndio Zetu Kuwakilisha 2005, Bang 2007, Hawatuwezi 2005, Bang Rmx 2008, Mchizi Wangu 2008, Hakuna Mahali Kama 2008, Hiphop 2008, Iko Wazi 2009, Mpango Mzima 2010, Wawiwo 2010, na Katikati 2010.

Baadaye kundi hio lilivunjika na G Nako akajipata kwenye kundi la Weusi ambalo hapo awali lilikuwa linaundwa na Joh Makini, Nikki Wa Pili, G Nako Lord Eyes na Bonta Maarifa lakini baadaye Bonta alijitoa kwenye kundi hilo.

Kwa muda wote wakali hao wameweza kutengeneza Hit kama Gere, Humu Tuu, Show Time, Nicome, Mdundiko na zingine nyingi.

G Nako ngoma ambazo amekuwa akifanya kuanzia Nako 2 Nako hadi Weusi na zile ambazo amefanya kama Sol Artist amefanikiwa kufanya kwa mitindo tofautitofauti, kama vile mtindo wa Hip Hop na Bongo Fleva, lakini pia amapiano.

G Nako alifanikiwa kusimama kama rapa na mashabiki wakaukubali uwezo wake. Desemba 3, 2012, alitoa wimbo wa Mama Yeyo ambao amemshirikisha BenPol. Na kwenye ngoma hiyo kapita kwa midondoko ya rap kitu ambacho kinafanya wimbo huo kuonekana classic mpaka leo.

Siyo hivyo tu, utakumbuka kwa asilimia kubwa nyimbo alizofanya chini ya Nako 2 Nako na Weusi, alizifanya kwa style ya rap. Kama ile Interlude iliyotoka July 2, 2020. Aidha miongoni mwa ngoma kali ni hii Arosto ya kwake G Nako Ft Chin Beez & Nikki Wa Pili ambayo ilitoka Mei 20, 2024.

"Nikaanza peleka round kwanza, nikamwendea kumuomba namba mamaa, nikamvuta chemba nikatema cheche kadhaa," alichana G Nako kwenye Arosto.

Ukiachana na michano G Nako anatajwa kama mmoja wa wasanii wenye uwezo mkubwa wa kuimba viitikio kwenye muziki wa Bongo Fleva na hilo limejionesha kwenye ngoma nyingi ambazo ameshirikishwa.

"Kanipa maarifa, yakanifanya difa, nikajipa sifa, kaziba nyufa namuita ye mfalme " aliimba G Nako kwenye kiitikio cha wimbo Mfalme.

Hata hivyo mkali huyu ni miongoni mwa wasanii ambao wameweza kuendana na kila soko la muziki ambalo Bongo Fleva imepitia.

Ndani ya miaka minne muziki wa amapiano umekuwa ukifanya vizuri Bongo na Afrika kiujumla. G Nako pia ni miongoni mwa wasaniii ambao wameufanya kwa viwango vikubwa Novemba 10, 2023 alishirikiana na Diamond Platnumz kwenye ngoma ya Komando ambayo ipo kwenye mtindo wa amapiano,
Komando ni miongoni mwa ngoma ambazo zimempa mafaniko makubwa G Nako ikiwemo kutazamwa zaidi ya mara Milioni 9 kwenye mtandao wa Youtube.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwake kufanya aina hii ya muziki, utakumbuka 2023 alishirikishwa na Jux kwenye wimbo wa Sugga Dady.

Maua Sama Octoba 31, 2024 aliwashirikisha G Nako, Jaiva & Ibra kwenye ngoma yake ya Kariakoo ambayo ni amapiano na G nako ndio alipiga kiitikio. Mpaka sasa imesikilizwa mara laki mbili ikiwa ni audio tu.

Lakini pia ameshiriki kwenye wimbo wa Kinamba Namba wa wa kwake Billnass ambao ulitoka Oktoba 3, 2024 pia ni amapiano. G Nako anaingia kwenye orodha ya wasanii wa Tanzania wenye uwezo mkubwa wa kuimba aina mbalimbali ya muziki.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags