Msemaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Alex Makaro, amethibitisha kupokelewa kwa mgonjwa ambaye pia ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Gift Stanford 'Gigy Money' hospitalini hapo.
Akizungumza na Mwananchi, Makaro ameeleza kuwa kwa sasa msanii huyo ameshapewa ruhusa hivyo hawezi kuzungumza chochote kumhusu.
“Taarifa ni za kweli alikuwa anahudumiwa Muhimbili lakini tayari amesharuhusiwa leo kwa hiyo siwezi kuzungumzia chochote juu yake,”amesema Makaro,
Ikumbukwe kuwa Jumatano ya wiki hii Juni 18,2025, kulizuka taarifa kuwa msanii huyo amejeruhiwa vibaya na yupo katika chumba cha watu mahututi, lakini uongozi wa msanii huyo ulikanusha kuhusu taarifa hizo.
“Kwanza kuna habari inayosambaa kwamba Msanii Gigy Money, anaumwa ni kweli anaumwa na anahitaji maombi yenu sana, kuna wanaompigia simu na kwenda katika vituo vya afya mbalimbali kwani hapo awali kuna voice note ilikuwa ikisambaa kwamba yupo Goba au Massana hapana hayupo uko kote," imesema.
Pia uongozi huo umetoa pongezi na shukurani kwa madaktari wa hospitali mbalimbali zilizo jitahidi kumpa matibabu msanii huyo.
“Walijitahidi sana kumsaidia mpaka ilipofikia hatua yakupelekwa Muhimbili na pia tunapenda kuwashukuru madaktari na hospitali zote zilizojitahidi na kumpokea kipenzi cha wengi, tuseme Mungu ni mwema," imesema taarifa hiyo.
Hata hivyo, uongozi huo umekanusha taarifa zinazosema chanzo cha msanii huyo kuumwa ni baada ya kupigana na kupigwa.
" Ni kweli Gigy anaumwa lakini hajapigwa wala kupigana kwani habari inayosambaa mtandaoni kwamba kapigana au kapigwa ipuuzwe, huu muda anahitaji faraja, amani na mapumziko yupo kwenye kupambania maisha yake," imesema taarifa hiyo.

Leave a Reply