Msanii wa muziki wa Hip hop nchini, Msamiart ameweka wazi sababu inayofanya atumie majina ya waasisi wa taifa la Tanzania kwenye nyimbo zake.
Akizungumza na Mwananchi, Msamiart amesema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kuthamini mchango na alama walizoacha waasisi hao akiwemo Bibi Titi na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
"Kila mtu anaweza kuwa kiongozi lakini viongozi bora ni wachache, ambao wana maono na kusimamia vitu na wao ndio walifungua milango ya vitu vingi tulivyonavyo sasa hivi.
"Bibi Titi ndio alikuwa mwanamke wa kwanza kupigania uhuru kipindi ambacho kazi hizo zilikuwa zinaonekana za wanaume kabisa achana na sasa hivi wanazungumzia haki sawa.
"Pia kwa namna hiyo ndio tunazungumza na mama, dada, na mabinti zetu kuonesha wanawake ni zaidi ya kupika na kila kitu. Hamna namna nyepesi ya kuzungumza na kizazi kilichopita na kizazi kipya kikaenda vizuri kama sio kuzungumza vitu vinaweza kuwaunganisha wote kwa pamoja kama hizi ngoma," amesema Msamiart.
Aidha amesema hutumia lugha ya Kinyakyusa kwenye nyimbo zake kwa sababu anatafuta upekee kama msanii.
"Sio tu kwa kabila ni kupata kitu chako, kwa wasanii wote duniani ili kupata mafanikio makubwa lazima awe na kitu chake. Hata kwangu mimi ilikuwa lazima nije na kitu changu mimi, kwangu ni rahisi kutumia kwa sababu ndio lugha mama.
"Ukija mjini kila mmoja anatamani kuongea kwa swaga inakuchanganya utajaribu kuwa kimjini halafu utajichosha. Niliona najichosha bora nibaki kama nilivyo," amesema Msamiart.
Aidha, msanii huyo amewajibu wanaosema anatembea na upepo wa kufanya kazi nyingi na rapa Young Lunya akiwa na nyimbo mbili amemshirikisha. Amesema anafanya hivyo kwa sababu Lunya ndio rapa wa moto kwa sasa.
"Ingekuwa hivyo kila mtu angefanya kazi na Lunya lakini pia ukishafanya na Lunya hamna msanii mwingine mkubwa wa kufanya naye labda ufanye na Darassa. Lunya ndio msanii wa moto kwa wakati huu na mimi nafanya vitu vya moto kwa wakati huu, sio kwamba Lunya anafanya kazi na mimi tu kwanini wengine kazi zao hazionekani, ni rahisi kufanya na Lunya kwasababu mimi na yeye tunamuunganiko mkubwa," amesema Msamiart.

Leave a Reply