Jaji Ambadilikia Diddy Mahakamani

Jaji Ambadilikia Diddy Mahakamani

Jaji wa shirikisho anayeongoza kesi ya ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono dhidi ya Sean "Diddy" Combs, Jaji Arun Subramanian alimbadilikia msanii huyo na majaji wake baada ya Diddy kutoa ishara isiyofaa Mahakamani.

Wakati rafiki wa karibu wa Cassie, Bryana Bongolan alipokuwa akitoa ushahidi mahakamani Diddy alionesha ishara ya kutikisa kichwa kwa nguvu huku akiwaangalia majaji watoa uamuzi wa kesi yake ikiwa na maana kuwa ushahidi huo sio wa kweli.

Jaji Aruna alimtaka wakili mkuu wa Diddy, Marc Agnifilo kuzungumza na mteja wake kwani jambo hilo halikubaliki kabisa Mahakamani. Ambapo Marc alikili jambo hilo kutojitokeza tena.

“Niliwaona mteja wenu akiwaangalia majaji na akitikisa kichwa kwa nguvu. Hilo halikubaliki kabisa. Ikijirudia tena, hata ikitokea mara moja tu, nitasikiliza ombi kutoka kwa serikali la kutoa maelekezo ya kurekebisha kwa majaji ambalo hutaki litolewe, Au nitazingatia kuchukua hatua zaidi, ambazo zinaweza kumfanya mteja wako atolewe mahakamani,”amesema Jaji Aruna

Aidha katika kesi hiyo shahidi mwingine muhimu aliyefahamika kwa jina bandia la Jane alipandishwa Mahakamani ambapo alieleza kuwa alianza uhusiano wa kimapenzi na Diddy mwaka 2020 lakini mambo yalibadilika na kuingizwa katika biashara za kingono.

Jane alieleza kuwa Diddy alitumia ushawishi wake, msaada wa kifedha, na vitisho kumdhibiti, na kwamba alijikuta akitengwa kijamii baaada ya kupokea fedha kutoka kwa Diddy huku akidai kuwa rapa huyo alimuhonga fedha ili abadilishe ushahidi wake.

Combs anakabiliwa na mashtaka matano, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono, njama ya uhalifu, na kusafirisha watu kwa ajili ya ukahaba. Iwapo atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Hata hivyo Diddy amekanusha mashtaka yote, akidai kuwa vitendo vyote walivyofanyiwa wanawake hao vilikuwa ni kwa ridhaa yao na kwamba madai dhidi yake ni ya uongo.

Utakumbuka Sean "Diddy" Combs alikamatwa Septemba 16, 2024 katika Hoteli ya Park Hyatt, Manhattan, New York na kupelekwa moja kwa moja katika gereza la Metropolitan huko Brooklyn. Kesi yake ilianza kuzikilizwa Mei 5,2025 huku mashahidi zaidi ya 15 wakitoa ushahidi akiwemo Kid Cudi, Mia, Cassie Ventura, mama mzazi wa Cassie, Bryana Bongolan na wengineo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags