Jumatatu nyeusi kwa mastaa Bongo Muvi, msiba wa Tesa

Jumatatu nyeusi kwa mastaa Bongo Muvi, msiba wa Tesa

Jumatatu nyeusi ya Novemba 4, 2024, hivi ndivyo unaweza kuiita kutokana na watu maarufu nchini kujitokeza katika Viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam wakiwa wamevalia mavazi yenye rangi nyeusi katika shughuli za kuuaga mwili wa aliyekuwa mwigizaji wa Bongo Muvi, Grace Mapunda ‘Tesa’ aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi Novemba 2, 2024.

Tesa alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, kwa maradhi ya nimonia yaliyomsumbua kwa takriban wiki moja. Mwili wake utazikwa leo saa 10 jioni katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Aidha katika shughuli hizo za kutoa heshima ya mwisho viwanjani hapo, mwili wake uliwasili saa nne asubuhi ukiwa umebebwa na wasanii wenzake akiwemo mwigizaji wa Tamthilia ya Juakali, Isarito Mwakalindile ‘Luka’, mwigizaji wa Huba Mrisho Zimbwe ‘Roy’ na wengineo huku wote wakiwa wamevalia mavazi meusi.

Mbali na wasanii wenzake, viongozi mbalimbali wa dini na Serikali nchini wamefika katika viwanja hivyo kutoa salamu za mwisho akiwemo Mtumishi wa Mungu Boniface Mwamposa, Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma “Mwana FA”,  na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Ikumbukwe kuwa Tesa alizaliwa Julai17, 1968 na kufariki dunia Novemba 1, 2024.

RATIBA YA MSIBA

Mwili ulifika Leaders saa 4:00 Asubuhi

Ibada ndefu saa 4:30 Asubuhi

Salamu za rambirambi saa 6:00 Mchana

Wasifu wa marehemu saa 7:00 Mchana

Neno la shukrani saa 7:30 Mchana

Kuaga mwili saa 8:00 Mchana

Mwili utapelekwa makaburini saa 9:30 Alasiri

Mazishi saa 10:00 Jioni






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags