Justin Bieber Achekelea Dili La Mkewe Hailey

Justin Bieber Achekelea Dili La Mkewe Hailey

Mwimbaji wa Pop kutoka Canada, Justin Bieber (31) ameonyesha kufurahia dili jipya la mkewe Hailey(28) lenye thamani ya Dola1 bilioni wakati huu ambapo anaripotiwa kukabiliwa na matatizo ya kifedha kutokana na kuandamwa na madeni.

Jumatano hii, Mei 28, Hailey kupitia Instagram alitangaza kwamba chapa yake ya urembo, rhode ambayo yeye ni Mwanzilishi na Mkuu wa Ubunifu, imeingia makubaliano ya kibiashara na chapa ya vipozi ya e.l.f. cosmetics.

"Nilipozindua rhode mnamo 2022, siku zote nilikuwa na ndoto kubwa kwa kampuni hii na jambo la muhimu zaidi kwangu ni kuendelea kuisogeza rhode karibu zaidi na ulimwenguni," alisema Hailey na kuongeza.

"Kwa hivyo, leo ninafurahi sana na ninajivunia kutangaza kuwa tumeingia makubaliano ya ushirikiano na e.l.f, hatua hii nzuri ni ukurasa mpya katika himaya ya rhode," alisema Hailey ambaye muda wowote anaweza kutangaza kufikia hadhi ya ubilionea.

Hailey ambaye kufuatia dili hilo anaenda pia kuwa Mshauri wa Kimkakati wa e.l.f, alisema anajisikia mwenye nguvu zaidi na msisimko kuliko hapo awali huku akiwashukuru wote ambao alishirikiana nao tangu awali wakati anaanza mradi huo.

"Shukrani kwa timu ya kipeke ya rhode ambayo imenisaidia kujenga chapa hii kwa miaka mingi. Nisingeweza bila ninyi nyote na washirika wote wa rhode. Asanteni kwa kuwa msaada katika safari hii, kwa pamoja hatua ijayo itakuwa moto zaidi," alisema.

Miongoni mwa mastaa waliopongeza ni pamoja na Kylie Jenner na Kim Kardashian ambaye utajiri wa Dola1.7 bilioni kwa sehemu kubwa unatokana na mikataba minono anayosaini kupitia chapa zake za mavazi na vipodozi.

Baada ya chapisho la Hailey, mumewe Bieber alichukua chapisho hilo na kwenda kuliposti katika ukurasa wake wa Instagram akiambatanisha na picha ya mrembo huyo ambaye ni mama wa mtoto wao mmoja.

Hayo yanajiri zikiwa ni wiki kadhaa tangu kuripotiwa kuwa mkali hiyo wa kibao, What Do You Mean? (2015), ana deni la mamilioni ya dola kutokana na kuahirisha ziara yake ya Justice mwaka 2022.

Ikumbukwe Septemba 2018, Bieber na Hailey ndipo walifunga ndoa ya kiserikali huko New York, wawili hao waliokutana kwa mara ya kwanza Novemba 2009 katika kipidi cha Today Show, walionekana mahakama ya Manhattan ambapo vyeti vya ndoa hutolewa.

Miezi miwili baada ya kufunga ndoa, Hailey alibadilisha majina katika mitandao ya kijamii na kuwa Hailey Bieber, na mwaka mmoja baadaye huko South Carolina, wakafanya harusi kubwa iliyohudhuriwa na watu zaidi ya 150 katika hoteli ya Montage Palmetto Bluff.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags