Kabla ya THT Barnaba, Amini, Young Dee walianzia huku

Kabla ya THT Barnaba, Amini, Young Dee walianzia huku

Mwaka 2006 liliandiliwa shindano la kusaka vipaji vya uimbaji lililopewa jina la 'Talent Show'. Shindano hilo lilikuwa na msisimko mkubwa kwani walijitokeza vijana wengi ambao walikuwa na ndoto ya kufanya muziki lakini hawakuwa na jukwaa la kuonesha vipaji vyao.

Katika shindano hilo walipatikana washindi ambao kwa kipindi hicho hawakuwa na majina na wengine walifika kwenye mashindano hayo wakiwa hawajawahi kurekodi. Lakini kwa sasa wamekuwa na majina makubwa na kuishika gemu ya muziki Tanzania.

Katika shindano hilo mshindi wa kwanza alikuwa Barnaba, wa pili Young Dee, wa tatu Amini na wa nne alikuwa Young Tuso.

Akizungumza na Mwananchi mwandaaji wa shindano hilo Nicoraus Shoo, amesema baada ya kuhitimu chuo cha Dar es Salaam School Of Journalism (DSJ), ndipo aliandaa shindano hilo ambalo mshindi wa kwanza mpaka wa tatu walipata nafasi ya kurekodiwa wimbo mmoja kwenye studio ambayo ilikuwa inafanya vizuri kwa wakati huo G Record.

"Nilifanya kama tamasha na shindano la vipaji na niliomba ukumbi, matangazo na zawadi ambayo ya washindi kurekodi kwenye studio za G Record. Nashukuru brother G Rapper alinipokea vizuri ambapo badala ya kutakiwa kurekodi mshindi mmoja nilipata nafsi ya washindi wote watatu ambapo mshindi wa pili na wa tatu walitakiwa kufanya wimbo wa kushirikiana," amesema Nicoraus .

Nicoras amesema kuna baadhi ya wasanii walienda kwenye mashindano hayo wakiwa hawana majina ya kisanii.

"Walikuja kwenye mashindano hayo wakiwa hata majina ya A.K.A hawana mfano Young Dee alikuja anaitwa David. unajua jina la Young Dee alipewa na Dully Sykes na hiyo ni baada ya kutoka pale kwenye mashindano. Barnaba alikuja na jina lake hilohilo baadaye ndiyo akaongezea Classic walikuja pale wametoka mtaani kabisa," amesema Nicoraus

Nicoras anasema shindano hilo liliwaandaa wasanii hao kwani baada ya kupata ushindi kwenye mashindano hayo, ndio akili ya sanaa ikaanza kufunguka na kuamini kuwa wanaweza.

"Walikuja pale kutafuta nafasi ya kurekodi tu, na baadaye Barnaba na Amini wakaenda kujiunga na THT. Pale kwenye mashindano kulikuwa na madansa wa THT kwahiyo wao ndio waliwaunganisha mpaka kufika THT," amesema Nicoraus .

Hata hivyo, amesema shindano hilo bado litabaki kuwa sehemu ya historia ya vipaji vya wasanii hao kwani lilisaidia kuwatengeza kuwa wasanii wazuri.

"Shindano ambalo niliandaa mimi kwa sababu nilianzisha na nikawa jaji. Lilikuwa la wiki nne mfululizo kwahiyo kuna vitu ambavyo tulikuwa tunaelekezana pale msanii akija unamwambia unavyoimba hivyo hautofika mbali badilisha hiki weka hiki.

"Bahati nzuri tulipata wasanii ambao wameweza kusimama mpaka leo wanamichango mikubwa. Yaani tukimuongelea Barnaba amekuwa zaidi ya msanii ni mwanamuziki sasa, Young Dee rapa mkali sana na Amini ni mwanamuziki pia kwa sababu anaimba live na anapiga vyombo," amesema Nicoraus .

Amesema hata baada ya wasanii hao kupata nafasi ya kurekodi lakini hawakufanya hivyo kwa sababu walikuwa wamepata mchongo wa kwenda THT.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags