Kama Vipi Tuzo Zitolewe Kila Mwezi

Kama Vipi Tuzo Zitolewe Kila Mwezi

Juzi kati nilikuwa mitaa ya kati. Nipo 'bize', natembea, nimevimbiana kama Aziz Ki mbele ya bibie Hamisa. Sina habari na mtu, sina hofu na maisha, sina pesa na mapenzi. Kifupi mimi ndo 'singomani' la taifa pasee.

Kwa mbali nikaona kadem flan hivi. Utembeaji wake ni kama nakajua. Yes! Kalipokaribia ni kweli namjua sana tu. Ni Kadigo kutoka mitaa ya Sahare Tanga. Unajua vitoto vya tanga vina mvuto wa pekee wenye upekee.

Nilikafahamu wakati huo nasoma pale Popatilal naye akisoma Usagara. Mimi nikiishi Nguvumali, na yeye akiishi na dada yake mitaa ya Chuda. Kalikuwa ka shemeji kangu kwa mtoto Zay yeye alikuwa akiishi Chumbageni.

"Jamani Levy mambo?" Kalisalimia huku kakisogea mwilini kuniwawo. Nami nikaitikia huku nikitanua mikono kama mwewe anayevamia eneo lenye vifaranga. "Shem Saumu, mambo vipi mtoto?" Kalikuwa kananunikia vizuri.

Ni mitaa ya Kijitonyama hapo. Ndipo nilipokutana na Saumu. Shida yake ni moja tu Saumu. Kulaumu kila bebe wake wakiachana. Saumu ni pisi ya maana, kosa anajifubaza sana kwa kutumia uzuri kama silaha.

Saumu ukimsifia tu kaisha. Ni kama anasubiri kusifiwa maisha yake yote. Na wana wanaruka naye na kumtema, toka tupo 'skuli' Tanga. Kuna washikaji wawili walikuwa wanangu, walimrukia na kumtema kwa nyakati tofauti.

Saumu hata ukimsifia mbele ya 'baby' wake, anavurugwa na akili. Hizo pigo huwakimbiza washikaji, hawadumu. Akiachika nina zali la kukutana naye. Nami hutafuta muda mzuri ili niweze kumshauri.

Safari hii tena aliniletea stori zake za kuachwa. Nikamchukua na kwenda naye sehemu tulivu ili nimpe ushauri wangu. Nikasogea naye kitaa Sinza, ushauri hutolewa kukiwa na mitungi. Wikiendi tena!

Ikabidi nimpe ushauri kwa kutumia mifano hai. Nilianza na wanasiasa, wanavyotumia mbinu wakitaka kura za wananchi. Mifano hii asipoweza kuelewa basi asubiri mauti tu, maana atakuwa na bichwa mfu.

Nilianza hivi tumebakiwa na muda mfupi kabla ya mbilinge na vurugu za uchaguzi. Ukipanga leo kugombea, umechelewa sana. Wenzako walianza mchakato toka Oktoba 2020. Biashara asubuhi jioni hesabu.

Chaguzi ni vituko na matumizi ovyo ya akili. Wabunge watarejea majimboni kulamba miguu ya wananchi. Kujitia unyonge, kujinyenyekeza kibwege ili kuaminisha watu kuwa ni mtu wa watu. Anayeguswa na shida zao.

Ataacha 'Joni Woka' na 'totozi' za Tabata, Sinza na Masaki. Kisha huyo 'bushi' kujichanganya na Wanyalu wa Mtwivira kugida nao ulanzi. Mwendo wa kuzungusha 'raundi' za ofa hata kwa mtu asiyemfahamu.

Hata watoto wadogo wa kike atawaita 'Mama' kwa adabu. Kama alihusudu na kukenua meno alipoitwa 'Mhe.' na raia. Sasa atalikataa jina hilo, atataka aitwe 'Mtumishi'. Unyenyekevu wake utamtisha mpaka shetani.

Wakati kabla alipita kitaani kioo juu na 'tintedi'. Sasa atatamani kung'oa na milango ili aonekane na kusalimia kila mtu. Kanisani, msikitini, viwanjani na vijiweni na popote ulipo msiba atafika na kusaidia kila kazi.

Atakuja na gia za kale. Kwa kuanzisha ligi za mpira. Kununua jezi za Kichina Kariakoo na kugawa kwa vikundi vya vijana. Na mambo ya 'Jimbo Cup' au 'Mbunge Cup'. Staili hii vijana hujikuta wanamfanyia kampeni bila kujijua.

Moja kati ya kesi mbaya kwa Mungu. Ambayo sisi ngozi nyeusi itatuponza. Siyo tu uzinzi na vinginevyo. Bali kwa matumizi mabaya ya akili. Tunatumia vibaya akili tulizopewa bure na Mungu baba Mwenyezi.

Upuuzi huu kila ukikaribia uchaguzi. Ni wa kawaida miaka nenda miaka rudi. Hatushituki na kuwapuuza wanasiasa wa hivi. Tunawachagua tena na tena. Ni matumizi mabaya ya akili. Masikini hutumia masikini kujitajirisha.

Miaka yote yupo Dar tunapishana kwa korido za Mlimani City. Kwenye kaunta za bar akishindana kulipa bili za tungi. Miezi kadhaa kabla ya uchaguzi ndipo anakumbuka jimboni lake. Anarudi 'bushi' kuuza nyago.

Mwaka huu wengi watarudi jimboni. Kupiga picha na kuzisambaza kwenye magazeti na mitandaoni. Kukodisha bodaboda au kutembea kwa miguu. Wakijifanya ni sehemu yao. Wanajua ni shida za miezi mitatu tu, uchaguzi ukiisha baasi.

Ni hii ngumu kupeleka maendeleo jimboni. Wanahonga wapate ubunge kisha hutoweka. Uchaguzi ukikaribia wanarudi kwa staili ile ile ya kuhonga. Na sisi kama mazuzu tunamatumizi mabaya ya akili, tunampa jimbo tena.

Hili ni hata kwa wasanii wetu. Kukiwa na tuzo wanakuwa wapole sana. Hapa ndipo utaona ukarimu wao hata kwa majibu yao kwa mashabiki. Nyodo na mbwembwe zao hutoweka kabisa na lugha yao ni "tuko pamoja bladi."

Kukiwa na tuzo ndipo simu za wasanii zinapatikana sana. Waandishi hupewa ushirikiano mzuri hata ibilisi akakosa soko la ufitini. Wasanii ni waungwana sana pindi wanapokuwa na shida na tuzo. Wakishapata wanarudi kwenye dunia yao.

Kimsingi 'politisheni' na 'myuzisheni' ni jamii moja. Kama ambavyo na wao hujinyenyekeza kwa raia wanapotaka kura za ubunge. Ni hulka moja na ile ya wasanii wakitaka kuachia wimbo au kugombea tuzo.

Kama kwenye soka tuzo zinatolewa kila mwezi. Itapendeza hata wasanii wakigombea tuzo kila mwezi. Namna hii itasaidia wasanii kuishi kiutu, kwa nidhamu na heshima. Maana wakati huo wote hugeuka malaika.

Ndivyo ilivyo kwa washikaji wakitaka penzi. Unyenyekevu na uungwana wao huwatisha mpaka vibwengo wa baharini. Wanaume ni kama wasanii na tuzo au wanasiasa na kujiuza kwa wapiga kura.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags