Wawili hao waliocheza pamoja filamu kama Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), wamefanya uamuzi huo muhimu baada ya kushindwa kumpata mnunuzi wa jumba hilo la Beverly Hills tangu walipoanza kuliuza kimya kimya Juni 2024.
Jumatano hii chanzo kimoja kimeliambia jarida la People kuwa ingawa tangu mwanzo walikuwa na matumaini makubwa ya kuuza nyumba hiyo, pia walikuwa na wasiwasi wa kupata hasara kubwa mbeleni.
"Walipunguza bei ili kuvutia wanunuzi zaidi, lakini walipoona hakuna mabadiliko, walipewa ushauri wa kuiondoa sokoni. Ulikuwa ni uamuzi wa kibiashara walioufanya pamoja," chanzo hicho kilidokeza.

Mtaalamu huyo wa masuala ya mali isiyohamishika, aliendelea kwa kusema kuwa soko la sasa ni gumu kwa wauzaji, hasa kwa mali za bei ya juu kama hiyo, hivyo kuisitisha kwa sasa hadi mazingira ya soko yawe rafiki kwa wauzaji ni uamuzi wa busara zaidi.
Ikumbukwe Lopez na Affleck walijaribu kuuza nyumba hiyo bila kuitangaza hadharani mnamo Juni 2024 kabla ya kuiweka wazi sokoni Julai mwaka huo, licha ya kuishusha bei kutoka Dola68 milioni hadi Dola59.95 milioni bado imekosa mteja.
Jumba hilo lenye vyumba 12 vya kulala, bafu 24, majiko 15, eneo la kuegesha magari 15, ukumbi wa sinema, bwawa la kuogelea, saluni, viwanja vya michezo n.k, lilinunuliwa na mastaa hao kwa bei ya Dola61.8 milioni ikiwa ni takribani mwaka mmoja wa ndoa yao.
Wawili hao walinunua jumba hilo hapo Juni 2023 baada ya kufunga pingu za maisha huko Las Vegas Julai 2022 ikiwa ni miaka 18 tangu walipoachana kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2004.
Hata hivyo, chanzo kimoja kilidokeza wakati huo kuwa Affleck, mshindi wa Oscar mara mbili, hakuipenda nyumba hiyo kutokana ipo mbali na watoto wake aliowapata katika ndoa na Jennifer Garner ambaye walidumu tangu mwaka 2005 hadi 2018.
Lopez aliwasilisha ombi la talaka kutoka kwa Affleck hapo Agosti 2024 baada ya miaka miwili ya ndoa. Waliendelea kuishi bila kutangaza rasmi kuvunjika kwa ndoa yao hadi walipoamua kuhitimisha rasmi uhusiano huo Januari 2025.
Kufuatia kuachana huko, Affleck alinunua jumba la Dola20.5 milioni katika eneo la Pacific Palisades hapo Julai 2024, na makazi haya mapya yapo karibu na watoto wake, Violet, 19, Seraphina, 16, na Samuel, 12, aliowapata na mkewe wa zamani, Jennifer Garner.
Naye Lopez, mkali wa kibao, On The Floor (2011), Machi mwaka huu alilinua nyumba ya Dola18 milioni 18 mjini Los Angeles. Kwa mujibu wa People, staa huyo alianza kutafuta nyumba kufuatia ndoa yake na Affleck kuanza kuyumba hapo Aprili 2024.
Utakumbuka Lopez na Affleck, awali walikuwa na uhusiano mwaka 2002 hadi 2004, walipoachana Lopez akaenda kufunga ndoa na Marc Anthony (2004 - 2014) na kujaliwa watoto wawili, huku Affleck akimuoa Jennifer Garner (2005 - 2018) na walijaliwa watoto watatu.
Baada ya kurudiana na kufunga ndoa hapo Julai 2022, Lopez aliliambia jarida la Vogue kuwa amebadilisha jina lake la mwisho baada ya kuolewa na Affleck. Alieleza kuwa watu bado watamuita 'Jennifer Lopez' ila jina lake halalini 'Mrs. Affleck', lakini sasa ndio hivyo kila mmoja ana maisha yake.
Leave a Reply