Kampuni ya Mwananchi ni mwendo wa kidijitali zaidi

Kampuni ya Mwananchi ni mwendo wa kidijitali zaidi

Dar es Salaam. Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Victor Mushi amesema lengo la kuweka nguvu katika uzalishaji wa maudhui mtandaoni ni kufungua wigo kwa walaji na kuwapa uhakika wa kupata kile kinachozalishwa na MCL wanapokihitaji.

Ametoa kauli hiyo leo Januari 23, 2024 katika mahojiano na Clouds FM alipozungumzia mabadiliko yaliyofanywa na MCL, yakiwamo ya namna ya upatikanaji wa taarifa kupitia tovuti zinazomilikiwa na magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Kupitia maboresho yaliyofanyika kwenye tovuti hizo, baadhi ya habari zitamhitaji mtu kulipia kiasi kidogo cha fedha ili kusoma uchambuzi wa kina uliofanyika ndani ya habari husika.

“Sasa tunatengeneza njia mpya ya biashara kwa hiyo hatutakupa kila kitu bure, lazima uchangie kitu kidogo. Kuchangia huku kunaiwezeka kampuni kuendelea kukupatia kilicho bora,” amesema Mushi.

Amesema mabadiliko hayo na kurahisisha upatikanaji wa maudhui kwa njia ya mtandao (dijitali), hakuondoi upataji habari kupitia nakala ngumu za magezeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Amesema gazeti la The Citizen pekee ndilo litakuwa na mabadiliko ambayo yalianza kushuhudiwa tangu Januari 9, 2024 kwa kuacha kuchapishwa Jumamosi na Jumapili.

“Ilikuwa mara saba kwa wiki, sasa lipo Jumatatu mpaka Ijumaa. Jumamosi na Jumapili linapatikana kwenye tovuti ya gazeti hilo kwa ujazo na uzito uleule. Hii ni moja ya mkakati wa jumla wa kujenga uwezo wetu wa kuandaa maudhui na kusambaza kupitia mifumo ya dijitali kwa sababu huko ndiyo dunia ilipo,” amesema Mushi.

Amesema maudhui biashara yake ni mnyororo wa thamani kwa kuwa lazima yatafutwe, yachakatwe, yaongezwe thamani, yasambazwe, mawazo ya walaji (feedback) yachukuliwe na kufanyiwa kazi ili kuyaboresha zaidi.

“Hizo zote ni fursa, kuna watu wanafanya shughuli hizo, kuna wadau ambao pia wanafanya shughuli hii,” amesema.

Mhariri Maudhui Mtandaoni wa MCL, Zourha Malisa amesema kupitia mabadiliko hayo, watumiaji wa tovuti za Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen sasa watakuwa wakichangia kiasi kidogo cha fedha ili kusoma habari zote za kina ikiwamo maudhui maalumu (Prime content).

Ili kufanya hivyo, mtumiaji wa tovuti hizo atatakiwa kulipia Sh500 kwa siku, Sh3,000 kwa wiki, Sh15,000 kwa mwezi na Sh91,000 kwa mwaka mzima.

“Tunapatikana mitandaoni kila siku, siku ambazo hujapata gazeti la The Citizen katika nakala ngumu utalipata mtandaoni na huko tunaongeza thamani katika habari zetu kwa kuweka video na infographics ambavyo ingekuwa ngumu kuvipata katika gazeti,” amesema Malisa.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags