Hali ya mwanamuziki wa Singeli Msaga Sumu imeendelea kuimarika ikiwa leo ni siku ya tatu tangu apate ajali na kufikishwa Taasisi ya Tiba na Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI).
Hayo yamesemwa leo Mei 19, 2025 na meneja wake Khalid Khalid wakati akizungumza na Mwananchi Scoop.
"Kwa sasa yupo sawa anatembea. Ila bado tu majeraha madogo madogo kwa sababu amevunjika mbavu moja kulia na nne kushoto. Ila kidogo hali yake ni tofauti na tulivyokuja.
"Leo tunasubiria vipimo kwa daktari kwa sababu anarudishwa tena kufanyiwa uchunguzi tunasubiri majibu yatavyokuja ndiyo tutajua, yupo sawa zaidi au laa. Lakini kiafya na kisura tunavyomuona sisi tunaona yupo sawa, tusubiri vipimo vituambie ndani yupoje kwa sasa bado yupo Moi,"amesema meneja wa msanii huyo.
Utakumbuka Msaga Sumu alipata ajali Mei 16,2025 wakati akirejea Dar es salaam akitokea Wilayani Namtumbo kutumbuiza kwenye mkesha wa Mwenge.
Aidha awali akielezea chanzo cha ajali hiyo, Meneja Khalidi alisema “Wakati tunarudi bodaboda alikatiza mbele yetu kwa hiyo dereva katika kumkwepa ndio kuna kitu akaparamia tukapinduka mara tatu. Kwa sasa hali yake sio mbaya yupo vizuri madaktari wanashughulika naye tunasubiri majibu ya moja kwa moja kutoka kwa daktari,” alisema.
Msaga Sugu amewahi kutoa nyimbo kama vile Unanitega Shemeji, Cheupe Dawa, Kiki, Mambo Bado, Vikoba na nyinginezo akiwa anatajwa kama muasisi wa Muziki wa Singeli nchini.

Leave a Reply