KONTAWA na harakati za muziki

KONTAWA na harakati za muziki

Ebwana eeeh, hii ni Ijumaaa tulivu kabisa. Karibu sana kwenye makala za burudani ambapo wiki hii nakukutanisha na kijana machachari wanamuita ‘Kontawa.’ Bila shaka utakua unamfahamu kijana huyu hususani ukiwa unafuatilia masuala ya burudani.

Yap kwa majina yake halisi aliyopewa na wazazi wake anatambulika kama Abdu Hamid, maarufu kwa jina la ‘Kontawa’, msanii wa kizazi kipya ambaye amekuwa akifanya poa katika siku hizi za karibuni.

Naaam hii inafahamika bwana kupitia ngoma yake ya ‘Champion’ ambapo alimshirikisha Emmanuel Elibariki maarufu kama ‘Nay wa Mitego’ huku Remix akimshirikisha Rajab Abdul maarufu kama ‘Harmonize.’

Kibao hicho ambacho kimepokelewa vizuri mtaani na wadau mbalimbali wa muziki wa Hip Hop Tanzania, kwa kupigwa katika sehemu tofauti za starehe.

Ni ukweli usiopingika kwamba Kontawa kwa sasa ni miongoni mwa wasanii bora, wanaofanya poa katika upande wa muziki wa miondoko ya kufoka ambayo hutambulika kwa jina la ‘Hip Hop’, amedhihirisha hivyo kwa kutoa nyimbo ambayo imekuwa gumzo kwa kusikika katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

 

Sababu za kuandika ngoma hiyo.

 Kontawa anasema wazo la kuandika ngoma ya Champion ni baada ya kuona muziki wake unasikilizwa na watu wengi, hii ni baada ya kupata nafasi ya kwenda Iringa na kukuta watu wengi wanamjua sana na wanasikiliza nyimbo zake.

"Nilipata nafasi ya kwenda Iringa, nilivyopanda kwenye jukwaa kutumbwiza nilipokelewa kwa furaha kubwa sana ndipo nilivyoamini kuwa mimi ni mshindi (champion), na sio msanii mdogo," amesema.

 

Anasema baada ya kuona hivyo, alipata wazo la kuandika nyimbo hiyo kuwaelezea watu kutokujichukulia kawaida kwa vitu vidogo wanavyovifanya kwani kila hatua wanayoipiga kwao ni ushindi.

“Nikaamua kuandika nyimbo hii, kutokana na hatua niliyopiga katika tasnia ya muziki wa Hip Hop, huku nikiwaelezea watu kutokujichukulia poa kwa mambo muhimu wanayofanya,” amesema.

Anaendelea kueleza huku akisema kwa mara ya kwanza aliandika nyimbo hiyo yote mwenyewe na hakuwa na wazo la kumshirikisha msanii yoyote, lakini Ney wa Mitego aliposikia huo wimbo alimuambia angependa aweke baadhi ya mistari katika wimbo huo kutokana na kuwa na uhalisia wa maisha yake aliyopitia huko nyuma.

“Kwangu mimi niliona ni kitu kikubwa kutokana na ushawishi alionao Ney, kwa kuimba nyimbo zinazoelezea jamii, na niliamini kupitia yeye wimbo utazidi kwenda mbali,”

Lakini mwisho wa siku kitu kilichotoka kilikua ni kikubwa, kwani hata mimi nilionekana sijabebwa kutokana na aina ya mistari niliyoiandika kwani ilikubalika na watu mbalimbali.

Sababu ya kufanya remix na Harmonize

Kontawa anasema sababu ya kufanya remix na Harmonize ni kutokana na ukubwa aliokuwa nao, ndio maana hata alivyofatwa na Harmonize ili wafanye remix wa wimbo huo hakusita kufanya maamuzi.

“Alinitumia meseji katika mtandao wa Instgram, na kunieleza nataka tufanye kitu katika huu wimbo, nataka ufike mbali kwasababu una kipaji na unafanya vizuri, maneno hayo yalitosha mimi kukubaliana nae na kufanya remix,” amesema.

 

Akiendelea kufunguka, Kontawa anaeleza muziki ulikuja baada ya kukaa nyumbani bila ya kuwa na shughuli yoyote, kwani malengo yake ilikuwa ni kuendelea na masomo ya chuo baada ya kumaliza kidato cha nne, mwaka 2014.

“Nilikuwa natamani sana kuwa Mhandisi wa mapambo ya nyumba, hivyo sikupata fedha ya kwenda kusomea mambo hayo ndipo nikajikita kwenye muziki.”

Kazi aliyowahi kuifanya hapo awali

Anasema kabla ya kuwaza kufanya muziki pia alishawahi kuuza nguo za mitumba akitoa Kariakoo huku akipeleka Karume, wakati mwingine alikuwa anafanya kazi za viwandani.

“Nimefanya kazi kama hizo ili nipate ridhiki, lakini ujira ulikua mdogo uisokidhi baadhi ya mahitaji, ndipo nikaamua kujikita katika muziki na ndipo safari yangu ilipoanzia,”

Kadhalika anasema baada ya kutoa vibao kadhaa kama Sura ya baba, Mwanamke, Moyo, Mke, Shetani akisafiri alipokelewa poa katika gemu ya Hip Hop.

Scoop tuliendelea kupiga stori na Kontawa huku akifunguka kuwa hana msanii mmoja anayemtazamia kama Kioo ‘role model’ kwani anapenda kuzingatia uandishi mzuri kutoka kwa wasanii wengine wengi wazuri.

Hata hivyo ametueleza mbali na muziki hakuna kitu kingine anachofanya kwa sasa ila analo wazo la kufungua kampuni itakayo jihusisha na mambo ya mapambo ya nyumba ‘Decoration’ kwa sababu alikua na ndoto ya kuwa mhandisi kuhusu masuala hayo hivyo bado ndoto inaishi ndani yake.

Pia ameweza kueleza muziki wake anauuza kwa njia gani, ambapo ametueleza kwamba, “Kwa upande wangu naamini katika kuuza muziki wangu kwenye mitandao kama boomplay, sportfy kwa sababu fedha unaipata kule nitofauti na yule anaye uza moja kwa moja,”

Kontawa ambaye alianza muziki mwaka 2019 anasema kuuza muziki katika mitando kama ya Boomplay na Spotify, hela unaiona kutokana na watu wanavyopakuwa mara nyingi nyimbo yako kwa kuisikiliza hivyo yeye sio muhumini wa kuuza muziki kwa kutumia CD.

Ebwana eeeh nikukumbushe tu mdau kupitia kijana Kontawa hii dunia haihitaji watu wazembe kujituma, kupambana na kutokukata tama,a ndio unyama kwenye maisha sasa. Chukuo hiyo and have a nice weekend.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags