Maisha ya Tausi Mdegela, kulala kitandani kwake adhabu

Maisha ya Tausi Mdegela, kulala kitandani kwake adhabu

Msanii wa filamu na mfanyabiashara Tausi Mdegela anasema kutokana na kimo chake kifupi, kuna baadhi ya watu katika jamii na mitandao wanaona hastahili kufanya baadhi ya vitu.

Hayo ameyasema wakati akifanya mahojiano na Mwananchi na kuongezea kuwa kwa sasa amezoea kudhihakiwa.

“Nikitaka kufungua mlango ndio nakumbuka mimi ni mfupi, naanza kumuita dada yangu wa kazi anifungulie, nje na hapo sijiwazii kimo changu, napenda kufanya kazi kwa bidii na siangalii uigizaji pekee,” anasema.

Anasema licha ya kumiliki kitanda kikubwa analazimika kulala chini kwa ajili ya kuepukana na hekaheka za kupanda kitandani.

“Nina kitanda kikubwa lakini godoro naweka chini kwa sababu siwezi purukushani za kupanda na kushuka, lengo langu la kukinunua ni kumfanya binti yangu azoee mazingira hayo ili akienda kwa watu asione vitu vigeni.

“Ukiachana na kitanda ndani kwangu hakuna viti vya kukalia, nimeweka zuria na mito kwani siwezi kujitesa kupanda juu, nimeamua kujikubali nilivyo, nitaishi maisha ya furaha na siyo kufurahisha watu, pia nikitaka kushona nguo nakata mita mbili,"anasema

Hataki unyonge kwa binti yake

Tausi amejaaliwa kupata mtoto wa kike jina lake Pavitrah, anasema kipindi cha nyuma alipokuwa akienda kucheza na wenzake walikuwa wanamtania na kumwambia mama yake ana mwili mdogo na mfupi, jambo ambalo lilikuwa linamuumiza.

“Pavitrah mwanzoni alikuwa anakuja kusemelea anavyotaniwa na wenzake ananiambia mama wanasema wewe una kamwili kadogo na mfupi, nikawa namwambia mwanangu ni kweli mimi ni mfupi, ila nakupenda sana wakikwambia tena wajibu ndiyo mama yangu mfupi ila ni staa kuliko mama zenu.

“Siku moja akaenda kucheza wakaanza kumtania akawajibu kama nilivyomwambia, akarudi akanimbia mama nimewaambia kama ulivyonifundisha hawajarudia kunitania tena,"anasema

Changamoto za huduma za kijamii

Anasema kuna wakati akienda kupata huduma za kijamii sehemu zenye majengo ya ghorofa kwake inakuwa changamoto, kwani anaona kuna umbali mrefu kupanda ngazi.

“Hata kama kuna lifti lazima niwe na mtu ambaye anaweza akanisaidia kubonyeza zile namba za lifti kwani siwezi kufikia zilipo.Changamoto nyingine ninayoipata nikitaka kutoa pesa ATM sifikii kwenye mashine ile, hivyo nakuwa namuomba bodoboda wangu ama dereva bajaji anayeniendesha.

Sasa hiyo ni hatari muda wote kumtajia mtu namba yako ya siri, nashauri wahusika kwa kuwa mashine za kutolea pesa zinakuwa mbili moja waweke ya watu wafupi, ili na sisi tuwe na uhuru wa kutunza pesa zetu,"anasema

Nje na hilo anasema kwake inakuwa ngumu kuvuka barabara, kwani inakuwa shida kuonekana na magari marefu.

Jamii inavyomchukulia

Anasema kuna baadhi ya watu hawamchukulii kama binadamu anayestahili uhuru wake na kufanya anachokipenda, anakutana na changamoto ya kudharaulika kutokana na ufupi wake kupitia mitandao ya kijamii, huku wengine akiwasikia wakimsema vibaya.

“Unakutana mtu anasema huyu naye kwa nini anavaa hivi, sasa nakuwa najiuliza kwa nini wasivae wao vile wanavyoona nastahili kuvaa mimi, siku moja nilipanda basi nikawa naseng’enywa na wamama kwa kiluga cha kihehe, hawakujua mimi ni kabila lao, nikanyamaza kimya baada ya kufika kituo ninachoshuka nikawajibu kwa kihehe sijajiumba mwenyewe ni mpango wa Mungu, ikabidi washuke kuniomba msamaha,” anasema.


Aombwa msamaha baada ya umaarufu

Anasema kipindi anajitafuta alikutana na kitu kilichomkatisha tamaa, lakini akajikaza na kuweka nguvu kujaribu ishu nyingine ili mradi mambo yaende.

“Niliunganishwa na mtu ambaye nilikuwa namuomba nafasi ya kuigiza, baada ya kufika eneo ambalo nilihitaji kukutana naye, nikapiga simu akapokea kisha akasema ndio wewe uliyesimama hapo nikamjibu ndio, akasema hakuna kazi kiukweli niliwaza mengi sana.

“Nikaondoka huku moyo wangu ukiwa na huzuni, nikampigia simu rafiki yangu alikuwa Tanga nikamwambia nahitaji niwe mnenguaji akasema sawa njoo Tanga ujaribu maisha.Baada ya kufika huko rafiki yangu aliniambia anafahamiana na mzee King Majuto (marehemu), ataniombea nikaigize naye, akampigia na kumuelezea ishu yangu akamwambia twende kwake, baada ya kufika pale akasema mmekuja na nguo za kuigizia, baada ya stori za hapa na pale na kazi ikaanza siku hiyo hiyo,"anasema Tausi

Anasema hakuishia hapo akaanza kuishii nyumbani kwa Mzee Majuto.

"Alinilea kama binti yake na kipindi hicho alikuwa maarufu sana, basi alikuwa akikutana na wasanii anawaambia huyo ni mwanangu mpeni nafasi ya kufanya kazi, nikawa napewa kipaumbele, katika maisha yangu sitakaa nimsahau yule mzee, apumzike kwa amani,”anasema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags