Maisha yanavyowabadilisha wasanii

Maisha yanavyowabadilisha wasanii

Licha ya kuwa katika ulimwengu wa burudani, umaarufu na mafanikio mara nyingi hutafsiriwa kama kipimo cha furaha kwa wasanii, lakini wapo baadhi ambao wamekuwa wakiikimbia tasnia hiyo kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiimani, kifamilia, afya na mazingira.

Hilo linatukumbusha tarehe 12-08-2016 muda mfupi baada ya kumaliza swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ilala Bungoni (Masjid Taqwa), mwanamuziki wa Taarab, Mzee Yusuph alitangaza kuachana na kazi ya usanii na badala yake ameamua kumrudia muumba wake.

Lakini licha ya kutangaza hayo mwaka 2020 alirudi tena kwenye kazi za sanaa alizokuwa akifanya awali kwa kudai kuwa ameona pengo kwenye muziki huo. Kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Wakati naanza muziki huu wa kidunia, nilikuwa nina mori kuliko Mmasai, ila muda ulipokwenda mori ikapungua kisha nikaacha kwa kuwa nilihisi sioni sababu ya kuendelea, cha kushangaza sasa hivi nina hamu ya kuimba balaa, nataka niimbe mpaka nigaragare mwaka huu,” alieleza wakati anataka kurudi kwenye gemu.

Mbali na Mzee Yusuph, mwanamuziki Suma Lee ambaye aliwahi kutamba na ngoma kama vile 'Hakunaga', aliamua kuachana na muziki na kuhamia kwenye maisha ya kiroho huku akidai hata kazi zake ambazo bado zipo studio hatozitoa tena na kwenye vyombo vya habari zisipigwe.
Si hao tu hata kwa upande wake mwanamuziki Vannesa Mdee mwaka 2020, kupitia Podcast yake ya 'Deep dive with Vanessa Mdee' alitangaza kuacha muziki kwa madai ya kuwa sanaa hiyo inafanya akabiliane na msongo wa mawazo kwa muda mrefu.

"Nimekuwa nikiishi kwa nje najificha lakini ndani nakufa, nilikuwa siwezi kulala hadi ninywe pombe. Sina hamu tena ya kufanya muziki, sina hamu tena ya kuhudhuria shughuli yoyote ya kupokea tuzo, kuanzia sasa sitajihusisha tena," alisema Vanessa ambaye alichukua uamuzi huo baada ya kuwa katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka 10.

Hayo yaliyotokea kwa wasanii hao kuacha muziki ndiyo yametokea pia kwa mwanamuzi Snura Mushi ambaye jana Julai 29, 2024 litangaza kuacha muziki kwa lengo la kumrudia Mungu huku akitoa katazo la kazi zake kuchezwa kwenye vyombo vya habari.

Akizungumzia matukio ya baadhi ya wasanii kuacha muziki, mwanamuziki kongwe Joseph Francis ‘Mandojo’ amesema muziki una mambo mengi na ndiyo maana baadhi ya wasanii wanaamua wanaacha.

“Sababu za kuacha zipo nyingi lakini watu wengi wanaingia bila kujua mambo yanayoendelea ndani yake kwa hiyo wanapoingia na kuyagundua ndiyo wengine wanaacha.
"Kingine ‘industry’ yetu ya muziki Tanzania mambo mengi bado hayajakaa sawa.

Kwa hiyo mtu mwingine anaona anapata umaarufu na jina kubwa lakini hela hamna, hivyo anaona bora aachane na muziki afanye mambo mengine, pia unaweza ukaingia kwenye dini ukaona muziki kama vile dhambi ukaamua kuachana nao ndiyo maana sababu hazifanani,” amesema Mandojo.

Akizungumzia suala la wasanii hao kukataa nyimbo zao kupigwa kwenye vyombo vya habari, mtangazaji wa kipindi cha burudani ‘The Throne’ kinachoruka Crown Redio, Tony Sixteen amesema suala hilo ni gumu kwenye vyombo vya habari vilivyopo nje ya Dar es Salaam.

“Mtu kama Suma Lee alikataza kabisa watu kucheza ngoma zake kwa sababu ya dini japo ni ngumu sana kusimamia kitu kama hicho kwa sababu mara nyingi wanaoweza ni wale wa vituo vikubwa vya habari vya hapa mjini ambavyo vinajua kabisa vinafuatiliwa.

“Lakini ukienda kwenye media za mikoani ambako ngoma za wasanii zinachezwa ni ngumu sana watu kufuata maagizo ambayo yanakuwa yametolewa na msanii au laa, labda waende TCRA waombe barua rasmi ya kupeleka kwenye media zote liwe kama agizo ila nje ya hapo ni ngumu sana kusimamiwa,” amesema Tony.

Kuhusiana na msimao wa baadhi ya wasanii wanaofanikisha kuacha muziki Tony amesema kwa kipindi hiki ni kama kupishana na gari la mshahara.

“Ukiona hivyo ujue mtu kaamua kweli kwa sababu sasa hivi gemu imekuwa biashara kubwa watu wanatengeneza hela kupitia muziki kwa hiyo ukiona mtu ameacha kutengengeza hela kupitia muziki hasa kipindi hiki ambacho unalipa kuliko zamani ujue kaamua kweli ni kama kupishana na gari la mshahara.

“Mimi namuheshimu sana mtu anayeweka maamuzi magumu kama hayo kwa sababu hiki ndicho kipindi ambacho muziki unalipa zaidi kuliko kipindi chochote ambacho tumewahi kufanya muziki," amesema.

Kwa upande wake Dj Cobo amesema kuwa kauli hizo za wasanii kuacha muziki na kisha baadaye kurudi kwenye gemi huwa zinawachanganya.

“Hivi vitu vinatuchanganya kama Mzee Yusuph alisema hivyohivyo sasa hivi karudi watu wanatandika ngoma zake na yeye mwenyewe anaimba kwa hiyo tunawasikiliza wanavyosema badaye wakirudi tunapiga.

“Akitaka kuziruhusu akirudi tutapiga kwa sababu huyo anaona tukipiga tunamkumbusha labda alikuwa na matendo mabaya ya nyuma,” amesema Cobo.

Anachosema mtaalamu wa saikolojia
Aidha mtaalamu wa masuala ya saikolojia Dr. Magolanga Shagembe amesema kawaida binadamu hufanya mabadiliko kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kimazingira.

“Kwenye maisha ya mwanadamu kuna nafasi ya mabadiliko kwa kila mmoja wetu na hayo mabadiliko yanatokana na sababu nyingi inawezekana ni mtu binafsi anaona maisha aliyokuwa anaishi hayampendezi tena na watu wengine wanaomzunguka lakini inaweza kuwa ni msukumo wa ndani na msukumo kutoka nje kama vile maisha au kupata marafiki wapya, mpenzi ambaye anafanya abadili namna ya maisha.

“Kingine ni baada ya mtu kuwa amefanya kazi kwa muda mwingi na kufahamu faida na hasara kisha akagundua kuwa hasara ni nyingi kuliko faida, hapo anaweza kuamua kuepukana na mfumo wa maisha aliokuwa nao mwanzo," amesema.

Mashabiki wanavyosema
Mariam John mkazi wa Bagamoyo amesema wasanii wanatakiwa kufanya uamuzi wenye uhakika na siyo baadaye kubadili mawazo yao.

“Wasanii wanatuchanganya wanavyotoa mawazo ya kuacha muziki basi waache kweli kwa sababu wengine wanatoa mawazo ya kuacha kwa kukurupuka kisha siku kadhaa wanasema wanarudi tena jambo ambalo linatuchanganya,” amesema.

Prisca Emmanuel mkazi wa Mbezi Beach amesema baadhi ya wasanii wanatangaza kuacha muziki kabla ya kumaliza ujana jambo linalopelekea baadaye kubadili misimamo yao.

“Wasanii wanawahi kufanya uamuzi kwa sababu tumeona wengi ambao wanatangaza baadaye wanarudi kwa kutoa sababu kibao, lakini kama ilivyokuwa kwa Suma Lee ilikuwa kweli, wengine wanachanganya tu wanatoa maamuzi wakiwa na ujana ndani yao,” amesema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags